Makamu M/Kiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini Mhe. Seif Khamis Gulamali na Katibu wa kamati hiyo Bi. Felister Mgonja
pamoja na wajumbe wa Kamati tajwa hapo juu, wakifuatilia kwa makini maelezo ya
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya
Wizara ya Nishati Kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara kwenye Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini leo tarehe 20 Januari, 2021 Bungeni jijini
Dodoma. Kulia kwa Waziri Kalemani, ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
Mha. Leonard Masanja.
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini imempongeza Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard
Kalemani kwa kasi ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa zaidi ya
asilimia 80 ya vijiji vyote nchini vimepelekewa huduma ya umeme.
Pongezi hizo zimetolewa
na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.
Seif Khamis Gulamali baada ya Taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu Muundo na Majukumu
ya Wizara ya Nishati kuwasilishwa kwenye kikao cha Kamati hiyo tarehe 20
Januari, 2021, bungeni jijini Dodoma.
Mhe. Seif Khamis
Gulamali amesema kuwa, kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa na yawezekana
Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika katika usambazaji wa umeme vijijini.
Akizungumza kufuatia
pongezi hizo, Waziri Kalemani amesema, Wizara ya Nishati itahakikisha vijiji
vyote 2200 vilivyobakia ambavyo bado havijaunganishwa na umeme, vitapatiwa
huduma hiyo ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.
Akijibu swali kuhusu
maeneo yenye changamoto ya ukatikaji wa umeme hapa nchini, Waziri Kalemani
ameeleza kuwa, kwa upande wa Dodoma , Dar-es-salaam na Mwanza, Wizara ya
Nishati kupitia TANESCO imefunga mitambo yenye uwezo wa kutoa umeme wa kutosha
hivyo endapo kutatokea kukatika kwa umeme,
kutakuwa kumetokana na hitilafu za kiufundi.
Aidha, Waziri Kalemani
amekiri kuwa, kulikuwa na changamoto ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma isipokuwa eneo
la Masasi na Tunduru na kueleza kuwa kuna vifaa vya kuboresha nguvu ya umeme (
Automatic Voltage Regulators - AVR ) vinaendelea kufungwa ili kuongeza umeme
uwe mkubwa kwa ajili ya watumiaji.
Aliongeza kuwa,
ufungaji wa vifaa vya AVR unafanyika pia katika Jimbo la Nyasa na utakuwa
umekamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa na hivyo upatikanaji wa umeme
katika maeneo husika utaimarika.
Akijibu swali kuhusu
ratiba ya utekelezaji wa kazi za Wakandarasi wa umeme katika maeneo
yanayopitiwa na miradi ya umeme, Waziri Kalemani amesema, "tumewasihi sana
Wakandarasi wanapofika kwenye maeneo husika, wakutane nanyi Waheshimiwa Wabunge
na Wakuu wa Wilaya. Kwanza, kutoa taarifa kuwa wameingia kwenye maeneo yenu
lakini pia wajue wanaanzia maeneo gani yenye kero ili kushauriana nao mahali pa
kuanzia. Tutakapokuwa tunazindua tutawakabidhi kwenu Wakandarasi hao ili mkae
nao wajue waanzie wapi." Amesema Dkt. Kalemani
Akielezea kuhusu
upatikanaji wa mafuta kwa maeneo ya vijijini na miji midogo, Dkt. Kalemani
ameieleza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, Wizara ya
Nishati ina mpango wa kuendelea kusambaza vituo vya mafuta katika maeneo ya
vijijini na miji midogo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya Mafuta
na usalama kwa watumiaji wa maeneo tajwa.
Waziri Kalemani
amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa suala hilo, kanuni zinapitiwa ili
kupunguza gharama za uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na
miji midogo ili kuweza kupata wawekezaji wengi kwenye maeneo hayo.
Ameongeza kuwa, Wizara
ya Nishati, inafikiria kujenga vituo rahisi vya pampu moja, ambavyo uwekezaji
wake utakuwa nafuu.
Vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini vilivyoanza jijini Dodoma tarehe 20 Januari, 2021, vinatarajiwa kukamilika tarehe 22 Januari, 2021.
No comments:
Post a Comment