Saturday, January 2, 2021

NAIBU WAZIRI MABULA ABAINI UBADHILIFU WA BILIONI 2.175 KATIKA ZOEZI LA URASIMISHAJI MOROGORO

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amebaini ubadhilifu wa zaidi ya Bilioni 2 uliofanywa na Wakufunzi wa Chuo Cha Ardhi Morogoro (ARIMO) na kumuelekeza Mkuu wa Chuo Huruma Lugala kumsimamisha  kazi mara moja Mkuu wa Utawala wa Chuo Michael Lori kwa  tuhuma ya kushirikiana na wakufunzi wawili wa chuo hicho waliofanya ubadhilifu katika zoezi la urasimishaji.

Dkt Mabula alitoa maelekezo hayo tarehe 30 Desemba 2020 mkoani Morogoro wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na uongozi wa mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Alisema, Wizara yake ilifikiri kushirikisha makampuni binafsi katika zoezi la urasimishaji ingerahisisha kazi ya kupima na kumilikisha wananchi maeneo yao lakini matokeo yake baadhi ya makampuni na watu wachache wametumia nafasi hiyo kufanya ulaghai wa kuchukua fedha za wananchi bila kukamilisha kazi ya urasimishaji.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Utawala katika Chuo cha Ardhi Morogoro ameonekana kushirikiana na watuhumiwa kwa namna moja ama nyingine na uamuzi wa kumsimamisha ni kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Awali Dkt Mabula alielezwa na Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala kuwa wakati uongozi wa chuo hicho ukifanya jitihada za kukiboresha chuo ikiwemo kudhibiti hujuma mbalimbali ilibainia baadhi ya Wakufunzi wake kujihusisha na kazi ya urasimishaji katika maeneo mbalimbali kwa kutumia jina la chuo kujipatia fedha.

Alisema, chuo chake baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kubainia udanganyifu kwa baadhi ya watumishi wake kiliamua kuwasimamisha Wakufunzi wawili kupisha uchunguzi na kuwataja watumishi hao kuwa ni Adolf Milungala anayetuhumiwa kujipatia shilingi Bilioni 1.9 na Hamis Abdalah Kindemile milioni 275 fedha zilizokuwa malipo ya urasimishaji katika mitaa 43 Morogoro.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Chuo cha ARIMO alisema wakati uchunguzi ukiendelea dhidi ya watuhumiwa, Mkuu wa Utawala Lori amekuwa akishirikiana na watuhumiwa kukwamisha uchunguzi na hata pale alipotakiwa kujieleza kwa barua alijibu kwa dharau na kuongeza kuwa hata alipoitwa na tume ya uchunguzi aligoma kwa kisingizo cha ugonjwa.

Naibu Waziri Mabula aliupongeza uongozi wa Chuo cha ARIMO kwa hatua ilizochukua za kuwasimamisha watuhumiwa kupisha uchunguzi na kusisitiza kuwa Wizara yake imeanza kuchukua hatua kwa makampuni yote yaliyoshindwa kukamilisha kazi za urasimishaji.

‘’ Kufuatia tukio hili halmashauri inatakiwa kuchukua hatua za kukamilisha upimaji katika maeneo ambayo watuhumiwa walichukua fedha na nimekiagiza Chuo cha Ardhi Morogoro kuhakikisha na kinafanya upimaji katika maeneo hayo’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, lengo la Wizara ya Ardhi ni kwamba mwananchi aliyetoa pesa apimiwe na apate haki yake ya msingi  ya kupatiwa hati na kusisitiza  kuwa hilo ni  onyo kwa makapuni yote yasiyotekeleza kazi kuchukuliwa hatua na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mbaula alionesha kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji maduhuli ya serikali katika mkoa wa Morogoro aliyoyaeleza kuwa hadi kufikia Desemba 2020 kiasi cha bilioni 2.3 pekee kati ya bilioni 11 ndicho kilichokusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 18.

Pia alisema mkoa wa Morogoro unadai takriban Trilioni 1.06 kutoka kwa wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya pango la ardhi na kubanisha kuwa watendaji wa sekta hiyo wamekuwa hawaoneshi juhudi zozote za kudai fedha hizo wakati wakijua kuna madeni makubwa.

Naibu Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, Wizara yake kwa sasa itakuwa ikiwapima wakuu wa idara za ardhi kwenye halamashauri na Maafisa Ardhi Wateule kwa vigezo vya utendahji ikiwemo makusanyo ya kodi na kusisitiza watakaoshindwa wataondolewa katika nafasi hizo.

Aidha, Dkt Mabula katika ziara yake mkoani Morogoro alikagua pia ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Wilaya ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) iliyopo Mvomero unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).Pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi kuonesha kuridhishwa na ujenzi wa miradi inayojengwa na  NHC katika maeneo mbalimbali alilitaka Shirika hilo  kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora na kwa gharama nafuu.

No comments:

Post a Comment