Naibu
Waziri Kilimo Hussein Bashe leo tarehe 7 Januari, 2021 ameagiza Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Chamwino kuanza mara moja
uchunguzi dhidi ya Viongozi wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Zabibu
(CHABUMA AMCOS) katika wilaya hiyo; Waliochukua fedha kiasi cha shilingi
milioni 150 ambazo zimetumika kinyume cha utaratibu.
Naibu
Waziri Bashe amefika katika kijiji cha Buigili na kufanya mazungumzo na
Wawakilishi wa Wakulima waliokusanyika katika shamba lao la zabubu katika
kijiji cha Mwegamile kata ya Buigili halmashauri ya wilaya ya Chamwino ambapo
amemwagiza Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Chamwino kuchukua hatua stahiki
baada ya kuelezwa kilio hicho na Wakulima hao.
“Mhe. Mkuu
wa wilaya; Naomba uchukue hatua na kwakuwa Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU
Chamwino yupo hapa. Hawa Viongozi wachunguzwe na hatua stahiki zichukuliwe.
Tuziapate fedha za Wakulima wetu kiasi cha shilingi milioni 150.” Amekaririwa
Naibu Waziri Bashe.
Wakulima
hao wamemwambia Waziri Bashe kuwa CHABUMA AMCOS ilipokea fedha hizo kutoka kwa
Kampuni ya ARCO Vintage mwaka 2020 kwa lengo la kuboresha miundombinu ya sehemu
ya shamba hilo ili Kampuni hiyo iendelee kununua shehena ya zabibu kutoka
katika shamba la Wakulima hao lakini kinyume na utaratibu Viongozi hao
walitumia fedha hizo kwa mambo mengine.
CHABUMA
AMCOS ni Ushirika wa Wakulima zaidi ya 961 ambapo imeelezwa kuwa kuanzia mwaka
2010 kwa hiari yao walianzisha shamba la zabibu lenye ukubwa wa hekari 296
ambapo walipata mkopo wa bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya
umwagiliaji pamoja na uwekezaji mwengine ambapo ulichangia shamba hilo kufikia
uzalishaji wa juu wa zao la zabibu mwaka 2013 kiasi cha tani 600.
Tangu mwaka
2017 uzalishaji wa zabibu katika shamba hilo uliendelea kushuka na kusababisha
Wakulima kutelekeza mashamba yao na kusababisha uzalishaji kusimama kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo adhabu ya riba kutoka Benki ya CRDB kuendelea
kuongezeka, kupungua kwa mapato kwa Wakulima pamoja na kukosekana kwa uongozi
thabiti pamoja na usimamizi duni.
Katika
kukabiliana na hali hiyo Naibu Waziri Bashe ametoa maelekezo kadhaa ili
kurejesha hali ya uzalishaji katika shamba hilo.
Naibu
Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji kupeleka
Wahandisi kuanzia kesho tarehe 8 Januari, 2021 ili washirikiane na Wahandisi wa
halmashauri ya Chamwino kufanya tathmini ya gharama ya miundombinu ya
umwagiliaji na kuiwasilisha mara moja kwake.
Agizo
lingine ni Timu hiyo ya Wahandisi kufanya tathimini kama Mradi huo huo unaweza
kutumia nishati ya jua (Solar system) katika kuendesha mashine za kuvuta maji
yanayotumika katika kilimo cha umwagiaji katika shamba hilo.
Waziri
Bashe ameagiza kila Mkulima ahakikishe anasafisha kipande cha shamba lake ndani
ya shamba hilo; Kazi hiyo inatakiwa kukamila ndani ya siku thelathini kuanzia
leo (Tarehe 7 Januari, 2021).
Taasisi ya
Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) imeagizwa kufanya tathmini ya idadi kamili ya
miche ambayo itahitaji kwa ajili ya kupandwa baada ya sehemu kubwa ya miche
mingi kufa na wakati huohuo TARI inatakiwa kuanzisha kitalu cha miche ya zabibu
ambapo miche hiyo itatolewa bure kwa Wakulima wenye uhitaji wa miche hiyo.
Mhe. Bashe
amemtaka Mkuu wa wilaya kufanya mawasiliano na Meneja wa Shirika la Ugavi wa
Nishati ya Umeme (TANESCO) wilaya ya Chamwino kurejesha huduma umeme katika
shamba hilo kwa kuweka ‘transformer’ kama ilivyokuwa awali.
Agizo
lingine ni Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanda mafunzo ya
namna ya kuendesha Ushirika imara na endelevu kwa Wakulima wa CHABUMA AMCOS
ndani ya siku thelasini kuanzia leo (Tarehe 7 Januari, 2021).
No comments:
Post a Comment