Thursday, January 28, 2021

Chuo cha Uhasibu Arusha chasaini mkataba na TFF kuendeleza soka nchini


Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Shirikisho la Soka nchini (TFF) ili kuendelea kukuza michezo nchini.

Akizunzungumza mara baada ya utiwaji wa saini makubaliano hayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amepongeza hatua hiyo ya Chuo cha Uhasibu Arusha kuunganisha taaluma na sekta ya michezo hatua inayosaidia kulea, kukuza na kuendeleza vipaji katika michezo mbalimbali.

“Tutakitumia chuo hiki kama mfano kwa kufanikiwa kuunganisha mnyororo wa thamani kati ya taaluma na michezo, hatua hii ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine nchini ili kiuandaa wanataaliuma na wanamichezo ambao wataleta tija kwa taifa kwa kujiongezea vipato vyao na pato la taifa” alisema waziri Bashungwa.

Awali akiongea katika hafla hiyo fupi ya utiwaji wa saini ya makubaliano hayo Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Prof. Eliamani Sedoyeka alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuendeleza mitaala ya michezo hususan somo la uongozi wa soka kwa ngazi ya Cheti, Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili na hatimae hatiua ambayo itasaidia katika uanzishaji na uendeshaji wa shule ya uongozi wa soka.

“Mwaka ujao wa masomo wa 2021/2022, tumepanga kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana watakaofanya vizuri katika soka, na TFF watatusaidia katika kuwapata vijana hao, chuo kitawapa ufadhiri wa masomo kwa upande wa ada na malazi” alisema Prof. Sedoyeka.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF Wales Karia alisema mkakati huo wa chuo cha Uhasibu Arusha ni jawabu la kusimamia na kuendeleza wanamichezo ambao walikuwa wanapotea baada ya kumaliza kidato cha nne au cha Sita.

No comments:

Post a Comment