Baadhi ya uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga, katika mkutano wao wa kwanza wa mwaka 2020/2021 uliyofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud
Kondoro, akiteta jambo na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga wakati
wa mkutano wao wa kwanza wa mwaka 2020/2021 wa baraza hilo, jijini Dodoma.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), umefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa
Majengo ya Serikali 85 nchi nzima yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni
142 ikiwamo miradi ya “Buni – Jenga”.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi)
Arch. Elius Mwakalinga, ameyasema hayo jjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa
mwaka wa 2020/2021 wa Baraza la Wafanyakazi wa wakala huo na
kusisitiza kuwa hiyo ni hatua kubwa kitaasisi lakini hatua hiyo haijawaondoa
moja kwa moja kwenye changamoto za kuchelewa kwa baadhi ya miradi ya ujenzi.
Mwakalinga ameutaka uongozi wa wakala kutazama kwa undani hatua gani walizofikia
katika utekelezaji wa majukumu yao hususani namna wanavyoweza kushughulikia
changamoto katika kila eneo la
kiutendaji.
“Hakikisheni mnajitathimini kwa kina bado kuna changamoto za
kuzifanyia kazi na Serikali yenu inawaamini katika utoaji ushauri na usimamizi
wa miradi ya ujenzi na usimamizi wa miliki za Serikali”, amesema Katibu Mkuu
huyo.
Aidha, ameupongeza Wakala kwa hatua nzuri waliyofikia katika
miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni
Kota jijini Dar es Saalam ambapo hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi.
Mwakalinga ameitaka TBA kuendelea kujali masuala ya
wafanyakazi kutoka sekta binafsi kwa kuzingatia kuajiri watu wengi kwenye
miradi ya ujenzi hususani walinzi, babalishe, mamalishe, watalaamu wa ujenzi,
mafundi, vibarua na wanafunzi wa taaluma zote kutoka vyuo vikuu ili kuinua
kipato cha mtu mmoja mmoja na kupunguza umaskini nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huo, Arch. Daud Kondoro, amemueleza Mgeni rasmi kuwa katika mkutano huo wajumbe wa baraza la wafanyakazi watapewa elimu ya “haki za mtumishi mahali pa kazi na wajibu wa mtumishi kwa mwajiri” ili iweze kuwasadia kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
No comments:
Post a Comment