Usiku wa Desemba 26, 2020 utakuwa ni mwendelezo wa
matamasha ya kufunga mwaka yanayowahusisha wasanii na wananchi katika
kuburudika na kusherehea mafanikio ya kazi za Sanaa nchini.
Tamasha la Muziki la Serengeti limekuja kunogesha Siku ya
kufungua zawadi ambapo linahusisha wasanii kwa lengo la kuwaletea watanzania
furaha, amani, utulivu, utu wema na udugu ambavyo ni tunu za taifa ambazo ni
nyenzo za kulisaidia taifa na Watanzania kufikia maendeleo endelevu.
Siku hiyo itawafanya watanzania kuwa na siku yenye bashasha
kufurahia kazi za wasanii wetu na kuenzi kazi zao ambazo kila mara zimekuwa
kioo cha nchi yetu na kimataifa. Ufundi wao wa kazi ya sanaa umekuwa msingi
adhimu wa kumfanya mtanzania na wapenzi wa muziki wa Bongo fleva kufikisha
fikra au mawazo ambayo yanasaidia kuelimisha, kuonya, kuburudisha na kufundisha
jamii.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo yenye
dhamana ya kusimamia sekta ya Sanaa ipo mstari wa mbele kwa kushirikiana na
wadau wengine kuratibu, kusimamia na kutekeleza tamasha la Serengeti Music and
Art Festival ambalo litakalofanyika Desemba 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru.
Kutokana na umuhimu wake, wamejitokeza wadau kadhaa ambao
wameunga mkono wazo la tamasha ambalo linalenga kuwaleta pamoja na
kuwaunganisha wasanii mbalimbali kupitia kazi zao za sanaa.
Wadau hao ni kampuni ya Multichoice, redio EFM, Clouds
media, redio 5, Peramiho DJ’s, Global TV, Elsewedy Electric, Shirika la Hifadhi
za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kampuni ya
Magazeti ya Serikali (TSN), Chanel 10, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Shirika
la Mawasiliano la Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na benki ya NMB, CRDB.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewathibitishia Watanzania
tamasha hilo limekuja muda mwafaka na ni tamasha la kipekee ambalo litawaleta
pamoja wasanii na wananchi.
Uamuzi wa kufanyika kwa tamasha hilo ni taswira ya uamuzi
mahiri alioutangaza Dkt. Abbasi Desemba 02, 2020 Jijini Dar es Salaam wakati wa
mkutano wake na wasanii wa tasnia ya filamu ambapo alisisitiza kuwa siku hiyo
itakuwa ni maalum kwa ajili ya kusherekea sanaa za Tanzania.
Hakika huu ni mwanzo mpya katika sekta ya Sanaa kuwa na
tamasha ambalo linawaleta pamoja wasanii wakongwe na chipukizi ili waweze
kubadilisha uzoefu hatua ambayo imekuwa na mwitikio mkubwa wa wasanii ambao
wamelipokea kwa furaha na kuthibitisha ushiriki wao.
Hadi sasa zaidi ya Wasanii 60 wamethibitisha kushiriki
tamasha hilo wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi Kipya (Bongo Fleva) wa sasa
na wazamani, wamuziki wa nyimbo za Injili, singeli, sanaa za maonesho kama
maigizo na sarakasi na pia filamu fupi za Bongo Movie.
Idadi hiyo ya wasanii inaleta taswira ya ushirikiano, Amani
na upendo miongoni mwao. Wasanii hao ni pamoja na Sholo Mwamba, Nandy, Mrisho
Mpoto, Christina Shusho, Kala Jeremiah, THT, Aslay, Becka Fleva, Shilole,
Chege, Snura, Jesca Mshama, Dogo Janja, Dulla Makabila, Baby Madaha, Stamina,
Meja Kunta, GoodLuck Gozbeth, Linah, Barnaba, Young Dee, Mabantu, Msechu, Pam
D, Msami, Madee, Whouz, Fid Q, Weusi, Maarifa, Rapcha, MoniCentralZone, Baddest
47 and Dully Sykes
Huku wasanii wanaowakilisha Bongo Fleva wa awali ni
Inspector Haroon, Matonya, Z Anton, Tunda Man, Kassim Mganga, TID, Feruz, Soggy
Dogg, Chid Benz, Mb Dog, Wateule, Wagosi wa Kaya, East Coast Team, TMK wanaume
na Mtafya na Nini
Kufanyika kwa tamasha hilo ni utekelezaji wa sera ya
kitaifa ya maendeleo ya Sanaa hatua inayosaidia kusisitiza matumizi ya maadili
ya kitaifa katika shughuli za muziki, sanaa za maonesho na ubunifu kwa jumla.
Tamasha hilo litaanza Saa 08:00 Mchana katika Uwanja wa
Uhuru mpaka Alfajiri na kiingilio ni Tsh. Shilingi 5,000 na fedha hizo
zinalipwa kwa mfumo wa N-CARD ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali
ikiwemo Maduka ya Sunderland Sports Wear-Mtaa wa Kariakoo/Nyamwezi, Merere
Sports Wear - Kariakoo Mkabala na Big Bon Msimbazi, Maduka ya Shafii
Dauda-Sinza Makaburini na Tabata, Maduka ya Vunja Bei-Sinza Madukani, Sinza
Makaburini na Kinondoni pamoja na Uwanja wa Uhuru ambapo kadi hizi zitakuwa
zikiuzwa muda wote kabla na siku hiyo ya tamasha. Lipia tiketi yako sasa
kupitia huduma za kifedha za M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money pamoja na T-Pesa.
Mapato na matokeo ya tamasha hilo yanatarajiwa kuwa chachu
ya kuendeleza mifumo ya kutambua wasanii katika kutekeleza shughuli za
maendeleo ya sanaa.
Aidha, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa burudani itaendelea Desemba 27, 2020 katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambalo linahusu kazi mbalimbali za Sanaa ikiwemo uchongaji, uchoraji, burudani za asili za sarakasi na ngoma. Tamasha hilo halitakuwa na kiingilio ambapo watu wote wanakaribiwa kufurahia ubunifu na kazi za Sanaa za maonesho.
No comments:
Post a Comment