Tuesday, December 8, 2020

MADINI YAJA NA MKAKATI WA KUIFUNGAMANISHA NA SEKTA NYINGINE KIUCHUMI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza jambo kwenye ufunguzi wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini uliofanyika tarehe 7 Disemba, 2020 Mkoani Morogoro.

Picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Afisa Kazi wa Mkoa na Wakuu wa Idara, Taasisi na Vitengo  kwenye ufunguzi wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini uliofanyika tarehe 7 Disemba, 2020 Mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema kuwa, Wizara hiyo imelenga kuhakikisha inaifungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine kiuchumi ili ziweze kukua, kufuatia mafanikio makubwa yaliyofanyika  ndani ya kipindi cha miaka 3 tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2017.

Prof. Msanjila ameyasema hayo  Desemba, 7 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini linalofanyika mkoani Morogoro.

Ameongeza kwamba, tayari sekta hiyo imeziwezesha sekta nyingine kukua kiuchumi   kutokana na mchango wake katika pato la taifa, ukuaji  wake kiuchumi  ikiwemo mchango wa sekta hiyo katika kuingiza fedha nyingi za kigeni mwaka 2019.

’’ Sekta ya Madini imewezesha Sekta nyingine Kukua.Mkakati wetu kwa Mwaka huu ni kuhakikisha tunaifungamanisha na Sekta nyingine kiuchumi ili zikue,’’ amesisitiza Prof Msanjila.

Ameongeza kuwa, mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na ushirikiano wa pamoja katika ya Wizara na taasisi zake na kueleza kuwa, ushirikiano huo uliiwezesha wizara katika Mwaka wa fedha 2019/2020 kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 528. 

Akielezea mwelekeo wa makusanyo kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, amesema hadi kufikia mwezi Novemba 30, 2020 tayari wizara imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 260  kati ya shilingi bilioni 526 iliyopangiwa kukusanya na kuongeza, ‘’ninaamini tutavuka lengo. 

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa wizara na taasisi kwa kuwezesha kufikiwa kwa mafanikio hayo na kueleza kuwa, mafanikio hayo yameondoa ombwe lililokuwepo awali kuhusu mtazamo hasi wa sekta husika. 

Akizungumzia mahusiano kati ya Uongozi wa Wizara na Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) amekitaka chama hicho kuwa chanzo cha kutatua migogoro na kupata ufumbuzi badala ya kuwa chanzo cha kutengeneza matatizo baina ya wizara na wafanyakazi. 

‘’Vikao hivi visaidie kutujenga na kutupeleka mbele, tuendelee kuhimiza uadilifu na uaminifu ili sekta hii iendelee kukua. Naishauri Menejiment kuwahamasisha wafanyakazi kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa majukumu. Lakini pia nataka kusema mlango wa watumishi kujiendeleza kielimu uko wazi,’’ amesema Prof. Msanjila. 

Pia, ametumia fursa hyo kumpongeza Waziri Doto Biteko kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Wizara ya Madini, huku akieleza kuwa, alishughulikia masuala ya sekta hiyo kwa utulivu na busara na kuongeza kuwa, watumishi  wa wizara wako tayari kufanya kazi na Naibu Waziri Mpya,Ndulane Francis Kumba ambaye ameungana nasi . Aidha, amempongeza aliyekuwa Naibu Waziri Stanslaus Nyongo kwa ushirikiano alioutoa katika kipindi chote alichofanya kazi na wizara. 

Kwa upande wake,  Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi Tawi la Wizara ya Madini (TUGHE), meiomba Serikali ya Awamu ya Tano kuifanyia kazi changamoto ya kutopandishwa mishahara, na vyeo watumishi ili kuwawezesha kuendana na gharama za maisha. 

Pia, ameuomba uongozi wa wizara ya madini kuendeleza mpango wa mafunzo ya watumishi ya muda mrefu na mfupi ili kuendana na kasi ya ukuaji  na mabadiliko ya teknolojia kwa lengo la kuwezesha kuboresha utendaji kazi. 

Ameongeza kuwa, chama hicho kipo tayari kupkea miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotoa majibu ya changamoto za wizara ili kuwezesha wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kusonga mbele. 

‘’TUGHE inatambua kuwa uongozi wa Wizara na Taasisi zake umeimarisha mfumo wa usimamizi na udhibiti wa madini na hivyo kuongeza mapato yanayotokana  na madini kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi shilingi bilioni 528 mwaka 2019/2020 , hivyo kuvuka lengo la makusanyo na kufikia asilimia 112 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 470,’’ amesema Manyama. 

Naye, Afisa Kazi Mkoa wa Morogoro Lana Nkaya amesema uwepo wa Baraza la Wafanyakazi mahali pa kazi  lipo kisheria kwani  linatoa nafasi kwa washiriki kujua taasisi imefanya nini, kujua changamoto na  kupata maoni, Ikiwa litatumika vizuri litaiwezesha wizara kufanya vizuri. 

Ameongeza kuwa, chombo hicho kinatoa fursa kwa wafanyakazi kufahamu majukumu ya taasisi, uongozi kupata maoni ya wafanyakazi na sehemu ya kufanya mashauriano.

No comments:

Post a Comment