Friday, December 4, 2020

KAMISHNA WA MADINI AZINDUA DUKA LA BIDHAA ZA MADINI LA TAWOMA

Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wachama wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) jijini Dodoma.

Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, akizungumza jambo mbele ya wanachama wa  Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) jijini Dodoma.

Kamishina wa Madini Mhandisi David Mulabwa  aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, amezindua Duka la bidhaa za Madini linalomilikiwa na Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA). 

Uzindu  huo umefanyika Novemba 3 katika Viwanja vya  African Dream  vilivyopo jijini Dodoma. 

Sambamba na uzinduzi huo, Kamishna Mulabwa ametembelea mabanda mbalimbali yanayoonesha bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini zinazotengenezwa na kuoneshwa  na chama hicho. 

Aidha, Kamishna  Mulabwa, amekipongeza TAWOMA kwa hatua nzuri kilichofikia katika kujiletea maendelo  ikiwemo kuwaelimisha wachimbaji wengine hususan  wanawake. 

“Ninawapongeza sana TAWOMA kwa juhudi zao wanazozifanya katika kuleta maendeleo kwenye sekta ya madini, pia nichukuwe fursa hii kuwashukuru TAWOMA maana wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wachimbaji wengine hususan wanawake”, amesema  Kamishna  Mulabwa. 

Katika uzinduzi huo, Kamishina Mulabwa ameahidi kufanya kazi   bega kwa bega na Chama  hicho ili kukisaida pindi kinapohitaji msaada kutoka serikalini. 

“Sisi kama Serikali tutakuwa bega kwa bega na TAWOMA na tuko tayari kuwasaidia pale mtakapo hitaji msaada kutoka Serikalini, karibuni milango iko wazi,” ameongeza Kamishna Mulabwa. 

Akitoa ufafanuzi kuhusu  Chama hicho kupatiwa mikopo, Kamishna  Mulabwa amesema,  tayari Wizara ya Madini imeshaanza kuzielimisha taasisi za fedha ili  ziweze kutoa mikopo ya vifaa na fedha kwa wachimbaji wadogo nchini ikiwemo TAWOMA ili kuwazesha kupata mikopo na waweze  kuchimba  kwa faida. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa TAWOMA aliyechaguliwa na chama hicho Desemba 3, 2020, Gilly Mtinda Raja amewashukuru wanachama wa TAWOMA kwa kumuamini na kumchagua yeye  kukiongoza chama hicho ambapo ameahidi  kuto waangusha na kuhakikisha chama hicho kinakua. 

Pia, Raja amemshukuru Kamishna wa Madini  kwa kuzindua duka  hilo la kimkakati la bidhaa zitokanazo na madini ambapo, ameomba  ushirikiano wa Serikali   ili Chama kiweze kufanyakazi kwa pamoja na kuwaletea wanawake maendeleo. 

Vile vile, amewahakikishia wanachama wa TAWOMA kwamba Serikali  itahakikisha chama hicho kina wawezesha wanachama wake ili wafanyekazi zao za uongezaji thamani madini na kuyapeleka sokoni kwa tija na kwa faida. 

Nae, Mwenyekiti mstaafu wa Chama hicho, Eunice Negele amesema, TAWOMA imeshaandaa mazingira mazuri ya kuhakikisha maduka ya TAWOMA yanayoshughulika na uuzaji wa bidhaa zitokanazo na madini yanafunguliwa nchi nzima.

No comments:

Post a Comment