Said Said Nguya, CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameendesha kikao cha siku moja cha majadiliano na Sekretarieti za CCM za wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ametoa rai kwa wanachama na wananchi wanaotapeliwa kwa ahadi ya kupewa ajira, uteuzi ama huduma yoyote kinyume cha utaratibu.
Kikao hiko kimefanyika leo tarehe 19 Desemba, 2020 katika Ukumbi wa NEC, Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma.
"Watu watakaotapeliwa kwa kisingizio kwamba kuna mgao unaletwa makao makuu, ama kuhusu ajira, kupandishwa cheo au uteuzi, hao wametapeliwa wao wenyewe, hakuna mtu katika uongozi wa sasa anayeweza akaleta hela hapa makao makuu, 'hayupo'."
Katibu Mkuu ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi na wanachama waliotapeliwa na viongozi na watumishi wasio waaminifu kwa kisingizio cha kupandishwa cheo, ajira ama kupata uteuzi.
Kutokana na hali hiyo, ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwadhibiti watu hao na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Aidha, katika hatua nyingine Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi kwa viongozi wa Chama walioshinda na walioshindwa katika uchaguzi wa Dola ambapo ameeleza kuwa,
"Kiongozi yeyote wa kisiasa wa kuchaguliwa ndani ya Chama wa ngazi yoyote ambaye amepata nafasi kwenye Dola, aachie nafasi na tutatoa utaratibu nchi nzima namna ya kujaza nafasi hizo kwa njia ya uchaguzi."
Amesisitiza kuwa, "Principle ipo palepale, hatuwazuii viongozi wa Chama kugombea, waliokosa warudi kwenye nafasi zao, waliopata wawaachie wenzao nafasi hizo za chama."
Kikao hiko, kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Dkt. Hawasi Haule Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Ndg. Godwin Mkanwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Mkoa wa Dodoma Ndg. Ismail Jama
Huu ni utaratibu wa CCM kuendelea kujisahihisha, kujijenga na kujiimarisha zaidi baada ya uchaguzi ili kuwa imara zaidi katika kuzisimamia serikali zake zote mbili katika kuwaletea maendeleo wananchi.
MWISHO
No comments:
Post a Comment