Friday, November 27, 2020

TANZANIA YAIPONGEZA AfDB KWA KUENDELEA KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango(kulia) akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), nchini Dkt. Alex Mubiru (kushoto), alipokuwa akimuaga  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)  baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu Jijini Abidjani, Ivory Coast.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),  nchini Dkt.Alex Mubiru (kushoto), akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango(kulia) alipokuwa akiagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu Jijini Abidjani, Ivory Coast

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philip Mpango(kulia) akimkabidhi zawadi ya kitabu Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), nchini Dkt. Alex Mubiru (kushoto), alipokuwa akimuaga  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)  baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki hiyo makao makuu Jijini Abidjani, Ivory Coast.

Serikali ya Tanzania imeipongeza Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuendeleza ushirikiano wao wa muda mrefu katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. 

Pongenzi hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango wakati akimuaga aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo. 

Dkt. Mpango alisema kuwa benki hiyo imekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi kutokana na mikopo mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa katika kutekeleza miradi ya kimkakati. 

“Dkt. Mubiru kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika amesaidia kusukuma fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati hapa nchini na katika miaka miwili aliyokaa hapa, Tanzania imeweza kunufaika na fedha za kutekeleza miradi yenye thamani ya takriban dola bilioni 2.5”, alisema Dkt. Mpango. 

Alisema miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na benki hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu jijini Dodoma ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma na kituo kikubwa cha umeme cha Zuzu. 

Dkt. Mpango alisema miradi mingine ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 260 kutoka Manyovu, Buhingwe, Kasulu hadi Kabingu mkoani Kigoma pamoja na mradi wa kuunganisha Mkoa huo na umeme wa gridi kuu ya Taifa. 

“Vile vile hivi punde Benki ya Maendeleo ya Afrika imeridhia kutoa dola milioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa kubwa la umeme kutoka mto Malagalasi ambao unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 45 za umeme kwa ajili ya Mkoa wa kigoma”, alibainisha Dkt. Mpango. 

Aidha, Dkt. Mpango alimuomba Dkt. Mubiru kufikisha salamu za Serikali ya Tanzania na watanzania kwa ujumla kwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kubainisha kuwa anaamini Mwakilishi Mkazi atakayeteuliwa atakuja kuendeleza pale walipoishia. 

Naye aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo nchini, Dkt. Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo, alisema anaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha miaka miwili alipokuwa nchini. 

Aliipongeza Serikali kwa kupiga hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kubainisha kuwa Tanzania inauthubutu wa kipekee linapokuja suala la maendeleo. 

Alisema kwa niaba ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hususani katika masuala ya miundombinu ya barabara na umeme.

No comments:

Post a Comment