Friday, November 13, 2020

RAIS MAGUFULI ALIELEZA BUNGE VIPAUMBELE SEKTA YA NISHATI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia pamoja na kulifungua rasmi Bunge hilo la 12 leo tarehe 13 Novemba 2020 jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameainisha vipaumbele katika sekta ya nishati kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, chini ya serikali aliyopewa dhamana kuiongoza kwa awamu nyingine ya pili.

Akilihutubia Bunge la 12 wakati akilizindua jijini Dodoma, Novemba 13 mwaka huu Rais Magufuli alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali yake imejipanga kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikishiwa nishati hiyo ambavyo alivitaja kuwa havizidi 2,384.

“Takwimu za hadi jana zinaonesha tumefikisha umeme kwenye vijiji 9,884 kutoka vijiji 2,018 mwaka 2016. Nchi yetu ina jumla ya vijiji 12,280,” alifafanua.

Aidha, Rais alieleza kipaumbele kingine kuwa ni kuimarisha miundombinu ya nishati na kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme nchini.

Akifafanua, alisema kuwa katika kutekeleza hilo, Serikali yake inakusudia kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Nyerere, litakalozalisha megawati 2,115 sambamba na kuanza ujenzi wa miradi mingine mipya ya umeme wa maji katika maeneo mbalimbali.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na utakaotekelezwa katika eneo la Luhudji (megawati 358), Lumakali (megawati 222), Kikonge (megawati 300).

Mingine ni ya umeme wa gesi asilia Mtwara (megawati 300), Somanga Fungu (megawati 330), Kinyerezi III (megawati 600), Kinyerezi IV (megawati 300) pamoja na miradi mingine midogo midogo.

Vilevile, Rais alibainisha kuwa makusudio mengine ya Serikali ni kuzalisha umeme megawati 1,100 kwa kutumia nishati jadidifu yaani jua, upepo na jotoardhi.

Aliendelea kueleza kuwa katika kipindi hicho, Serikali yake imepanga kukamilisha mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida – Arusha hadi Namanga pamoja na unaoanzia Iringa – Mbeya hadi Tunduma ambayo alisema itaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Kenya na Zambia.

Kuhusu maeneo ambayo hayaunganishwa katika gridi ya Taifa, Rais Magufuli alisema Serikali imepanga kuyaunga maeneo muhimu ya nchi ikiwemo Kigoma.

Aliongeza kuwa, katika kipindi kilichopita cha uongozi wake, Serikali ilitekeleza miradi mingi ya kusafirisha umeme na hivyo kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta hatua iliyowezesha kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 719 kwa mwaka.

“Miradi hii yote ya umeme itakapokamilika, siyo tu itatuwezesha kuwa na umeme wa kutosha na kuufikisha kwenye maeneo yote nchini, bali pia itatuwezesha tuwe na ziada ya kuweza kuuza nje. Pia, itasaidia kupungua kwa gharama za umeme.”

Akizungumzia sekta ndogo ya mafuta na gesi, Rais Magufuli alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaanza utekelezaji wa miradi ya kielelezo ya bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Aidha, alieleza kipaumbele kingine kuwa ni kuhakikisha mradi wa kusindika gesi mkoani Lindi, unaanza sambamba na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani, kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

No comments:

Post a Comment