Saturday, November 21, 2020

Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan Mgeni rasmi mashindano ya NBC Marathon

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo  kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Suyuph Singo akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu mashindano ya NBC  Marathon yatakayofanyika Novemba 22, 2020 Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Kushoto ni Meneja Mahusiano na Serikali wa Benki ya NBC Bw. William Kallaghe.

Meneja Mahusiano na Serikali wa Benki ya NBC Bw. William Kallaghe akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu mwitikio wa wananchi kushiriki katika mashindano ya NBC Marathon yatakayofanyika Jijini Dodoma Novemba 22, 2020 .

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika mashindano ya NBC Marathon yatakayofanyika Novemba 22, 2020 Jijini Dodoma ambapo pia atashiri mbio za Kilomita 5.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Suyuph Singo kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo leo Novemba 21, 2020 Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza  hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya mashindano hayo.

“Lengo la mashindano ya NBC Marathon ni kwa ajili ya kuchangisha fedha  kusaidia  mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kansa ya shingo ya kizazi katika hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es salaam” alisema Bw.Singo.

Mashindano hayo yatashirikisha wanariadha 3000 ambao wanaendelea kujisajili kwa njia ya mfumo wa kielektroniki na watakimbia mbio za kilomita 5, 10, 21 na 42 ambapo jumla ya sh. Milioni 45.4 zitatolewa kama zawadiwa kwa washindi wa mbio hizo.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano na Serikali wa Benki ya NBC Bw. William Kallaghe amesema kuwa maandalizi ya mbio hizo yamekamilika na njia zote zitakazotumika kwa mashindano hayo zimetambuliwa na kuthibitishwa na Shirikisho la Riadha Duniani kwa kukidhi vigezo  na tayari wamepewa cheti cha kutambuliwa na Shirikisho hilo.

“NBC ipo makini na mashindano haya na imeingia mkataba wa miaka mitano kudhamini mashindano haya ambapo mapato yake yanatokana na usajili wa wanaridha ambao ada yao ya usajili ni Sh. 25,000/= zote zitaelekezwa hospitali ya Ocean Road kuwahudumia wagonjwa wanasumbuliwa na tatizo la kansa ya shingo ya kizazi” alisema Bw. Kallaghe.

Aidha, amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha pia wanariadha kutoka nchi tatu ambazo ni Kenya, Malawi na Uganda ambapo washiriki 35  watashiriki na wote wamefanyiwa vipimo vya Covid-19 na hawana tatizo lolote.

No comments:

Post a Comment