Monday, October 19, 2020

OKASH AAPA KUTOLALA HADI KIELEWEKE, AZISAKA KURA ZA DK MAGUFULI STENDI, SOKONI, DALADALA, VILABU VYA POMBE

Mgombea Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash akiwaombea kura  Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli na Mgombea  Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa abiria katika Daladala jijini Dodoma jana.
Okash akimgawia mfanyabiashara picha ya Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli katika Stendi Kuu ya Dodoma.
Okash akiwa na baadhi ya wafuasi wa CCM katika Soko Kuu la Job Ndugai Dodoma.
Mama mfanyabiashara katika Soko Kuu la Ndugai Dodoma akimsikiliza kwa makini Okash aliyekuwa akimwaga sera nzuri za CCM na kushawishi kuipigia kura CCM Oktoba 28.
Okash akiomba kura kwa waendesha bajaji jijini Dodoma.
Mmachinga akiangalia  picha ya kampeni ya Dk. Magufuli aliyopewa na Okash.
Okash akiomba kura kwa wafanyabiashara ndogondogo
Okash akifurahi pamoja na mawakala wa ukataji tiketi za mabasi Stendi Kuu ya Dodoma, baada ya mawakala hao kufurahia ushawishi wake wa kampeni zake nzuri.
Okash akigawa picha ya Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli katika moja ya vibanda vya biashara jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash amesema hatokata tamaa hadi ushindi mnono kwa CCM upatikane, aahidi  kuendelea  na utaratibu wake wa kuzisaka kura mahali popote kwenye masoko, stendi za mabasi, vijiwe vya kahawa, Vituo vya bodaboda, bajaji, Mama Lishe, vilabu vya pombe hadi Saluni.

 Tangu ameanza kampeni hadi sasa Okash hajakata tamaa, amekuwa akihaha huku na kule kuzisaka kura za Mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wagombea Ubunge wa CCM na wagombea udiwani wa chama hicho.

katika kutimiza azma yake hiyo, Okash jana alitinga kuzisaka kura katika Stendi mpya ya kisasa ya Dodoma, ambapo alikuwa anaomba kura akiwaonesha picha za Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli  na Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.

Aliomba kura kwa abiria ndani ya daladala, kwa wafanyabiashara ndogondogo, kwenye migahawa, kwa watumishi wa mabasi wakiwemo madereva, makondakta na mawakala wa ukataji tiketi , kwa waendesha bodaboda na bajaji waliopo hapo pamoja na abiria waliokuwa wakisubiri usafiri. 

"Hadi kieleweke mpaka ushindi upatikane, sitolala wala sitaona haya kumuendea mtu yeyote au kundi lolote la jamii hata mpinzani nitamuomba kura kistaarabu ili Oktoba 28 mwaka huu wawapigie kura wagombea wa CCM chama chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo watanzania," alisema Okash kwa msisitizo.

"Nitaendelea kuzitafuta kura za wagombea wa CCM popote pale, nitakwenda kuzitafuta kwa wafanyabiashara sokoni, kwa Mama Lishe, Baba Lishe, vijiwe vya kahawa, saluni za kike na za kiume mpaka  kwenye vilabu vya pombe hadi ushindi mnono kwa CCM upatikane," amesema Okash wakati anazitafuta kura hizo kwa udi na uvumba. 

Baada ya kumaliza  stendi, alikwenda Soko jipya la Job Ndugai,  Dodoma ambapo pia aliomba kura kwa wafanyabiashara wa kike na  kiume  huku baadhi wakiomba kuachiwa picha za kampeni za Dk. Magufuli na Mavunde baada ya kupendezewa na kampeni za Okash walizodai zina mvuto na ustaraabu.

Mfanyabiashara Zainabu Ali aliyekutwa akiuza matunda na mboga mboga ndani ya soko hilo, ubunifu wa Okash wa kufnya kampeni kwa kuwafuata wapiga kura ni mzuri na unatakiwa uigwe na wanaCCM wengine ili Oktoba 28, wajipatie kura nyingi.

"Ukweli ni kwamba wafanyabiashara hatuna muda wa kwenda kwenye mikutano ya kampeni wala kuangalia kwenye luninga, lakini kitendo cha kufuatwa maeneo yetu ya biashara tunapata wasaa wa kuzielewa vizuri sera za chama husika na kushawishika kukipigia kura. Hongera sana binti kwa kazi yako nzuri  unafaa kuwa kiongozi," Zaibabu alimalizia kwa kumpongeza Okash kwa jitihada zake za kuitafutia CCM ushindi.

Mwishoni mwa wiki, baada ya  kufanya kikao cha ndani na wanawake  katika Kata ya Nhinhi Jimbo la Mvumi, Okash aliwaongoza akina mama kwenda kwenye vilabu vya pombe kuendelea kuzitafuta kura za wagombea wa CCM.

Okash anasema aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona asilimia kubwa ya wanaume hawahudhurii mikutano ya kampeni. 

Walipofika kwenye vilabu vya pombe ambapo asilimia kubwa wanywaji walikuwa wanaume vijana kwa wazee, Okash aliwasalimia kwa heshima za mila na desturi za kiafrika na kuanza kumuombea kura Dk. Magufuli, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde na Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Msafiri Mdandalu.

Alitumia fursa hiyo kuinadi Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa kuelezea mambo mazuri yaliyomo humo kuhusu yatakayotekelezwa katika jimbo la Mvumi, Mkoa wa Dodoma na jinsi wazee watakavyosaidiwa kupitia mfuko wa Tasaf, vijana, wanawake na walemavu kupata mikopo isiyo na riba.

Akielezea kuhusu tukio hilo la kushtukiza, Mzee Mathayo Mazengo mmoja wa wanywaji, alisema kuwa kwanza walistuka kuona kundi la wanawake wakiwemo pia wake zao wakiwaendea eneo walililokuwa wakistarehe, lakini baada ya Okash kuwaelezea lengo lao na kuwaomba kura kistaraabu walifurahi na kukubaliana naye.

Mazengo anasema, huyo binti (Okash), ni jasiri na mpambanaji mzuri, tena ana lugha nzuri ya ushawishi kiasi kwamba hata asiyeipenda CCM ni rahisi kukubaliana naye.

Tukio lingine alilolifanya Okash ni pale alipoambatana na Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) CCM Mkoa wa Dodoma, Sophia Kiwanga kwenda kuzisaka kura kwa Mama Lishe, Saluni za kike na kiume pamoja na vijiwe vya kahawa katika mitaa mbalimbali ya Jimbo la Chemba.

Pamoja na kumuombea kura Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, na wagombea wengine wa chama hicho,  lakini vilevile waliunga mkono biashara zao kwa kununua vyakula na kunywa kahawa huku wakimwaga sera pamoja na kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na mgombea huyo.

Okash na baadhi ya viongozi wa CCM walipita katika Kata mbalimbali za Chemba ikiwemo Kata ya Msaada, ambapo walikutana na watu wa kada tofauti, wakiwemo wazee, vijana, wanawake, Mama Lishe na wauza kahawa.

Wengi wa waliowatembelea na kuwaeleza mafanikio ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Dk. Magufuli, walifurahi kuwaona viongozi hao na kufarijika kwa kuthaminiwa, hivyo kuahidi kumpigia kura Dk Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

"Kitendo hiki cha kuzitembelea kada hizi hata sisi kimetupa faraja, ambapo licha ya sisi kuwaeleza mafanikio aliyoyafanya Dk. Magufuli, lakini hata wao pia walielezea na kutaja baadhi ya miradi mikubwa inayofanyika katika uongozi wake, ikiwemo; ujenzi wa barabara ya lami ya Dodoma-Manyara, kuunganishiwa umeme kwa gharama ya  27,000, ujenzi wa Reli ya kisasa ya Dar- Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma," alisema Okash.

Okash tayari amefanya mikutano ya kampeni ya ndani na hadhara kwa mafanikio na kuacha alama za ushindi kwa CCM katika Kata mbalimbali za majimbo ya Kondoa Vijijini, Kondoa Mjini, Chemba na Mvumi, Dodoma Mjini pamoja na kuhudhuria mikutano ya hadhara Chamwino, Kongwa na Bahi na Mpwapwa.

No comments:

Post a Comment