Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiwahutubia Wageni waalikwa wakiwemo Wakulima na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata pamba kilichozinduliwa leo na Naibu Waziri Kilimo, Mhe. Hussein Bashe Mjini Kahama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata pamba mjini Kahama leo.
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Mhe. Hussein Bashe mwenye mkasi, akiwa pamoja na Viongozi wa mkoa wa Shinyanga, Wizara ya Kilimo na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali akikata utepe kuashiria kuzindulia rasmi kwa kiwanda cha kuchakata pamba kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) leo mchana, tarehe 8 Oktoba, 2020 mjini Kahama; Kiwanda hicho kilisimama uchakati wa zao la pamba tangu msimu wa kilimo wa 2013/2014.
Naibu Waziri Wizara ya Kilimo Mhe. Hussein Bashe mwenye shati nyeusi akipata maelezo kutoka kwa fundi mitambo mara baada ya mashine za kiwanda cha kuchakata pamba kuzinduliwa leo mjini Kahama wengine ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald
Kusaya amewapongeza Wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (Kahama
Cooperative Union Ltd – KACU) kwa kuzindua rasmi kiwanda cha kuchakata pamba,
hafla iliyoongozwa na Mhe. Hussein Bashe, Naibu Waziri Kilimo, mchana wa leo
tarehe 8 Oktoba, 2020 katika mji wa Kahama.
Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya
amesema Wanachama wa Chama Kikuu cha KACU Ltd wanastahili pongezi nyingi kwa
kuwa mazingira hayakuwa rahisi kufufua kiwanda hicho na kuongeza kuwa Vyama
Vikuu vingine vinastahili kuiga mfano huo.
Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd
kimefanikisha jambo hili baada ya kuandaa mpango biashara kwa ajili ya kufanya
shughuli za uchakataji wa pamba ambapo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) kupitia mpango huo; Iliridhia kukikopesha Chama hicho, mkopo wa jumla ya
shilingi Billioni 4 ili kufanya ukarabati wa kiwanda, ununuzi wa pamba mbegu na
uchakataji wa pamba mbegu ili kuzalisha pamba nyuzi na pamba mbegu.
Aidha, Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
Chama Kikuu cha Ushirika cha KACU Ltd kilisajiliwa mwaka 1994 kwa hati ya
usajili namba 5,493 ambapo wakati hadi sasa kina jumla ya vyama Wanachama 116
na kwamba kufufua mashine hizo ambazo zilisimama tangu msimu wa kilimo wa mwaka
2013/2014 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uzalishaji mdogo wa pamba
pamoja na kushindwa kuhimili ushindani wa makapuni binafsi.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa
uanzishwaji wa kiwanda hicho; Uende sambamba na ongezeko la uzalishaji wa pamba
na tija.
“Ndugu zangu Wanaushirika na Wakulima, ili
kiwanda kiendelee kijiendeshe kwa tija ni lazima tuzalishe malighafi za
kutosha, maana yake ongezeni uzalishaji wa pamba mara mbili ya uzalishaji wa
mwaka huu, na anzeni kwa kutumia mbegu bora, tumieni mbolea na Watumieni
Wataalam wote, wakiwepo Maafisa Ugani”.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa ili
kiwanda kiendelee vizuri ni lazima pamba izalishwe kwa wingi ili kukifanya
kiwanda kijiendeshe kwa kipindi cha mwaka mzima.
“Ninyi wote ni mashahidi kuwa baada ya
mavuno ya pamba kuisha, viwanda vyetu wa vinafanya kazi kwa kipindi kifupi cha
miezi miwili hadi mitatu; Hii si sahihi ni vizuri viwanda vikaongeza usindikaji
kwa kipindi kirefu cha mwaka mzima; kuwa na kiwanda kama hiki cha Kahama chenye
uwezo mkubwa wa kusindika pamba nyingi zaidi ya kilo elfu 71 kwa siku.”
Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata pamba
mbegu kilo 68,825 hadi 71,693 kwa siku na kuzalisha robota 144 hadi 150 za
pamba nyuzi. Uwezo huo ni mkubwa na ambao unaweza kuchakata pamba zote
zinazozalishwa katika mkoa wa Shinyana kwa zaidi ya kilo 6,100,000 kwa msimu
mzima.
Katibu Mkuu kusaya ameongeza kuwa azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ni kuanzisha, kuendeleza na kufufua viwanda ambavyo
vilikua havifanyi kazi kwa muda mrefu na kwamba kuanza kufanyakazi kwa kiwanda
hicho ni juhudi ya Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa
kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) baada ya kuja na mpango wa kuanza
kufufua viwanda vilinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika katika zao la pamba
vilivyopo katika Mikoa ya Geita na Shinyanga.
Wakati huo huo Katibu Mkuu ametumia muda
huo kutoa onyo kwa Wabadhilifu wote wa mali za ushirika popote nchini
kuhakikisha wanarejesha mali za Wanachama wa Ushirika mapema kabla Serikali
haijachukua hatua.
Katibu Mkuu Kusaya amesema mali zote
zilizoibwa na kuporwa na Viongozi wachache wasio waaminifu, zitarejeshwa kama
ambavyo zimeendelea kurejeshwa maeneo mbalimbali kote nchini.
“Nataka niwahakikishie kuwa, kama kuna mali ya ushirika ilichukuliwe isivyo halali; Mali hizo zitarudishwa tu. Nitoe wito kwa Mwananchi yeyote aliyechukua mali ya ushirika isivyo halali popote nchi, atumie wakati huu kurudisha kabla hatujaanza kuchukua hatua kali na katika jambo hili Serikali haitakuwa na huruma.” Amemalizia Katibu Mkuu Kusaya.
No comments:
Post a Comment