Waziri wa
Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibari, Mhe. Hamad Rashid Mohammed amesema kuwa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inatekeleza kazi kubwa katika kutoa
haki za binadamu kwa kutoa ripoti ambazo zinahusu masuala ya haki za watu na
ameitaka kujikita zaidi kwenye masuala ya kijamii hususani unyanyasaji wa
kijinsia kwani ni tatizo kwa Zanzibar.
Akizungumza
na ujumbe wa watendaji wa juu wa Tume hiyo Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar,
Waziri Rashid alisema kuwa siku za nyuma utekelezaji wa haki za binadamu
hususani masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ilikuwa ni ngumu kwani utekelezaji
wa ripoti za tume hiyo zilikuwa hazifanyiwi kazi tofauti na sasa.
“Siku za
nyuma mlikuwa mkiandika, kutoa na kusoma ripoti lakini zilikuwa hazifanyiwi
kazi, sasa hivi kidogo utekelezaji wa ripoti mnazoandika na kuziwasilisha zimekuwa na msaada zaidi kwa
jamii, kwani haki za binadamu hasa unyanyasaji wa kijinsia wananchi wamekuwa na mwamko wa kutafuta msaada wa
upatikanaji wa haki baada ya chombo chenu hiki kufanya kazi kubwa ya
kuwaelimisha wapi wanaweza kupata msaada wa haki zao”, Waziri Rashid.
Alisema,
kuwa kuna maeneo Zanzibar ambayo wananchi wanahitaji kupata haki zao za msingi
hususani kwenye eneo la unyanyasaji wa kijinsia na ucheleweshwaji wa haki za
binadamu katika baadhi ya Taasisi za kutoa na kusimamia haki nchini.
Naye,
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema kuwa ziara yake
Zanzibar inalenga hasa kujifunza mambo mengi na kupata ushirikiano kwa Serikali
na Taasisi zake katika utekelezaji wa haki za binadamu nchini.
“Katika
ziara yetu hii tumejifunza mambo mengi sana na kila tulipoenda tumeambiwa mambo
mengi sana na tunatakiwa kuyafanyia kazi sisi kama tume ili kuwezesha wananchi
wa Zanzibar kupata haki zao za msingi kila panapohitajika”, Jaji Mstaafu
Mwaimu.
Alibainisha,
kuwa utekelezaji wa ripoti za tume hiyo hapo mwanzo ulikuwa mgumu lakini kwa
sasa hivi mambo yemebadilika na sasa kila mtu anatenda kazi yake ipasavyo hasa
akipokea ripoti hizo ambazo zimekuwa zikitolewa na tume hiyo kuhusu masuala ya
haki za binadamu.
Aliongeza,
kuwa tume hiyo inapita katika Ofisi za Serikali na Taasisi zinazotoa na
kutekeleza haki za binadamu ili kupata uhusiano na ushirikiano mkubwa kwa
Serikali na kuwezesha wananchi wote kupata haki zao katika masuala mbalimbali
ya kijamii.
No comments:
Post a Comment