Mkuu wa
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Bw.Richard Mganga.
Serikali
imetoa takriban Milioni 150 kukarabati miundombinu ya viwanja vya michezo
pamoja na ujenzi wa kisima cha maji katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya
ambacho ndio chuo pekee nchini kinachozalisha walimu wa sekta hiyo.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu, Mkuu wa Chuo hicho Bw.Richard Mganga amesema kuwa
katika kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
John Pombe Magufuli chuo kilipatiwa fedha hizo kwa ajili ya kukarabati viwanja
vinavyotumika chuoni hapo lengo ikiwa ni kukuza na kuendeleza Michezo nchini.
“Tunaishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutupatia kiasi hicho cha pesa ambacho
kimetusaidia kukarabati viwanja vya michezo vikiwemo vya mpira wa pete, mpira
wa wavu, mpira wa kikapu na mpira wa mikono ambavyo vinasaidia kufundisha
walimu wetu”,alisema Bw. Mganga.
Bw. Mganga
ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2020/2021 chuo hicho kimetengewa takriban
Milioni 300 kwa ajili ya kujenga madarasa matatu na hosteli moja ambazo zitasaidia kuongeza
idadi ya wanafunzi katika chuo hicho.
Kwa upande
wake mwalimu wa Chuo hicho Bw. Somo Ahmed Kimwaga amesema kuwa chuo hicho
kinatoa mafunzo ya michezo kwa ngazi ya Cheti na Diploma katika fani ya Uongozi
wa Michezo na Ualimu wa Uongozi katika Michezo kwa Waalimu kutoka halmashauri
zote nchini.
Ameongeza
kuwa chuo hicho kimezalisha wataalamu wengi katika michezo akiwemo Bw. Robert
Chitanda anayefundisha timu ya polisi Morogoro ambaye pia ni Mwalimu Msaidizi
katika timu ya Taifa pamoja na Bw.Alfred Selengia ambaye ni Katibu Mkuu wa
Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).
Chuo cha
Maendeleo ya Michezo Malya kipo katika Wilaya ya Kwimba Jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment