Saturday, March 7, 2020

Wizara ya Kilimo lazima tuongeze tija na uzalishaji ili kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda – Waziri Hasunga

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo uliofanyika Leo Tarehe 7 Machi 2020 Jijini Dodoma. Wengine Pichani ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Musabila Kusaya(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo wakifuatilia kwa karibu mkutano wa kazi ulioongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga uliofanyika Jijini Dodoma, leo Tarehe 7 Machi 2020.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Musabila Kusaya akifuatilia kikao kazi na Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo uliofanyika Jijini Dodoma, Leo Tarehe 7 Machi 2020.
Sehemu ya Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo wakifuatilia kwa karibu mkutano wa kazi ulioongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga uliofanyika Jijini Dodoma, leo Tarehe 7 Machi 2020.

Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga leo Tarehe 7 Machi 2020 amekutana na Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma na kusisitiza umuhimu wa Watendaji wa Wizara katika kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya Kilimo.

Waziri Hasunga katika mkutano huo amesisitiza umuhimu wa kuongeza nguvu katika eneo la masoko, uongezaji thamani mazao ya kilimo (Usindikaji) kwa kufanya hivyo; Wizara itawasaidia Watanzania kufikia uchumi wa viwanda sawa sawa na hamasa ambayo imekuwa ikitolewa na Rais wa Awamu wa serikali ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri Hasunga amekiri Wizara imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya masoko na ili kubaliana na changamoto hiyo Wizara imeanzisha Kitengo cha Masoko chini ya Idara ya Maendeleo ya Mazao ambapo itakuwa ikitafuta masoko ya mazao yote ya Wakulima.

“Masoko ni eneo ambalo tunapaswa kuweka nguvu ya kutosha, pamoja na masoko eneo la pembejeo za kilimo nalo ni muhimu ili tuhakikishe pembejeo kama mbolea zinawafikia Wakulima kwa wakati, kwa bei nafuu na sawa sawa na mahitaji yao” Amekaririwa Mhe Waziri Hasunga.

Waziri Hasunga pia amezungumzia eneo linalohitaji kupewa kipaumbele ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza nyuzi za pamba.

“Lengo letu ni kupunguza nguo za mitumba na kuuza pamba ikiwa imeongezwa thamani”. Amesisitiza Waziri Hasunga.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa ili kilimo kiweze kufanyika kwa manufaa na tija ni lazima kuongeza eneo la umwagiliaji.

“Katika kilimo cha umwagiliaji hatujafanya vizuri na lazima tuongeze nguvu kivitendo kwa kuongeza usimamizi na udhibiti”. Amesisitiza Waziri Hasunga

Waziri hasunga amesema maeneo mengine ya muhimu ambayo yanapaswa kutiliwa mkazo ni ushirika na usimamizi madhubuti wa Viongozi wa Vyama vya Ushirika; eneo lingine ni kuongeza usimamizi wa Maafisa Ugani kwa kuwandalia kanuni za usimamizi wa utendaji wao wa kazi za kila siku; kuandaa kanuni na miongozo katika masuala yote yanayohusu kilimo na ushirika kwenda kwenye Halmashauri zote ambazo kimsingi ndizo zinatekeleza masuala yote ya kilimo.

Akizungumza na Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma ikiwa ni siku moja mara baada ya kuapishwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Musabila Kusaya amewataka viongozi hao kushirikiana ili kufikia malengo ya wizara ya Kilimo kadhalika kuhuisha matakwa ya Mhe Rais katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Amesema kuwa ameteuliwa kufanya kazi hivyo watendaji hao panapo jambo la kuendeleza sekta ya kilimo wasisite kushirikiana naye kwa karibu.

MWISHO

No comments:

Post a Comment