Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa leo Machi 5, 2020 amekabidhi mkopo uliotolea na Benki ya CRDB wa matrekta manane aina ya Mahindra na majembe yake yenye thamani ya sh. Milioni 65 kwa Vyama Vinne vya ushirika vya wakulima wa mkonge mkoani Tanga. Pichani, Mheshimiwa Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa moja ya matrekta hayo Emmanuel Urio ambaye ni mkulima. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye shamba la mkonge la wakulima wadogowadogo la Mwelya Sisal Estate la Korogwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Machi 5, 2020 amekabidhi mkopo uliotolewa na Benki ya NMB wa matrekta 11 na matrela yake 22 yenye thamani ya sh. Bilioni moja, kwa Vyama Vinne vya ushirika vya wakulima wa mkonge mkoani Tanga. Pichani, Mheshimiwa Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa moja ya matrekta hayo Greyson Nyari , Mwenyekiti wa Vyama vya Mkonge Mkoa wa Tanga kwenye shamba la mkonge la wakulima wadogowadogo la Mwelya Sisal Estate la Korogwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua matrekta manane aina ya Mahindra na majembe yake yenye thamani ya sh. Milioni 65 yaliyotolewa kwa mkopo na Benki ya CRDB kwa kwa Vyama Vinne vya ushirika vya wakulima wa mkonge mkoani Tanga. Mheshimiwa Majaliwa aliyakabidhi matrekta hayo kwa wakulima kwenye shamba la mkonge la wakulima wadogowadogo la Mwelya Sisal Estate la Korogwe Tanga, Machi 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi matreka 19 yenye thamani ya sh. bilioni 1.520 yaliyolewa kwa mkopo na Benki za NMB na CRDB kwa ajili ya wakulima wa mkonge wanaounda Vyama vya Msingi (AMCOS) vinne vya kilimo cha mkonge.
Ameyasema hayo leo(Alhamisi, Machi 5, 2020) baada ya kutembelea eneo eneo la shamba la mkonge la wakulima wadogo Mwelya Sisal Estate na kujionea shughuli za za usindikaji mkonge na kukabidhi matrekta kwa wakulima.
Benki ya NMB imetoa matrekta 11 na matera 22 yenye thamani ya sh. bilioni moja na CRDB imetoa matrekta manane na majembe yake yenye thamani y ash. milioni 520.
Waziri Mkuu amesema zao la katani ni miongoni mwa mazao saba ya biashara nchini, hivyo amewahamasisha wananchi kulima zao hilo kwa wingi. “Maafisa kilimo hakikisheni mnawasaidia wakulima kuanzia hatua za awali za utayarishaji shama hadi mavuno hadi utafutaji wa masoko.”
Amesema lazima zao hilo liuzwe kwa mfumo wa ushirika, wanatambua kuna wakulima wakubwa, wadogo na wa kati wote wanatakiwa waratibiwe vizuri ili wanaohitaji waende kununua kwa mfumo huo na namna ya kuuza iwe ya ushindani.
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote inayolima zao la mkonge waratibu na kuwatambua wakulima wote katika maeneo yao wawasajili na kuwaunganisha katika ushirika ambao utasaidia katika kuwapa elimu na namna bora kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kupata pembejeo na zana za kilimo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amezipongeza benki kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwasaidia wakulima kwa kuwakopesha matrekta ambayo yatarahisha shughuli za kilimo cha zao hilo la mkonge.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa AMCOS wahakikishe wanatoa taarifa za mapato na matumizi kwa wanachama wao na pia hata wanapokopa mikopo wawajulishe wanachama na wasitumie vibaya madaraka yao na kula mali za ushirika.
Amesema vyama vingi vya ushirika vimekufa kutokana na kuwa na viongozi wasiokuwa waaminifu wanaoshiriki katika kufuja mali za ushirika. “Serikali itawafikisha mahakamani viongozi wote wa ushirika wasiokuwa waaminifu.”
“Viongozi kama mnafikiria kwenda kwenye ushirika kwa ajili ya kuondoa umasikini usichukue fomu na kama upo madarakani andika barua ya kujiuzulu leo. Tutafanya uchunguzi na tukikubaini tutakupeleka mahakamani, hatuna mzaha na fedha za wananchi. Tumedhamiria kurugudisha ushirika wenye tija kwa wananchi.”
Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba amesema awali mashamba hayo manane ya mkonge yalikuwa yanamilikiwa na Serikali na kisha waliyabinafsisha matatu na matano yakabakia chini ya Bodi ya Mkonge.
Naibu Waziri huyo amesema Bodi ya Mkonge waliwapa wakulima wadogo wayaendeleze lakini kwa kipindi chote cha miaka 14 kuanzia 2004 hadi 2018 walikuwa wanalima na mapato yote yalikuwa yakwenda kwa muwekezaji kutokana na mfumo uliokuwepo.
Naye,Mweyekiti wa Wenyeviti wa AMCOS za zao la mkonge mkoani Tanga za mashamba ya Magoma, Magunga, Mwelya, Hale na Ngombezi, Bw. AmGreyson Nnyari amesema AMCOS zao zina jumla ya wanachama 1,081.
Amesema kilimo cha mkonge kwa kuwashirikisha wakulima wadogo kilianza 1999 katika shamba la Mwelya na kuenea kwenye mashamba yay a Magoma, Magunga, Ngombezi na Hale ilipofika 2002 na muasisi wa mfumo huo ilikuwa Kampuni ya Katani Limited.
“Baada ya kampuni ya Katani Limited kuendesha mfumo huo kwa miaka 14 malalamiko mengi yalijitokeza kutoka kwa wakulima na kuonesha kuwa mfumo huo haukuwa rafiki kwa sababu mkulima alikuwa analipwa kiasi kidogo na fedha na kwa wakati anaotaka yeye licha ya mkulima kusimamia shughuli zote za shamba kuanzia hatua na uuandaji, upandaji, uvunaji na usafirishaji wa mkonge hadi kiwandani.”
Amesema baada ya malalamiko hayo ya wakulima kufikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Martine Shigela aliunda kikosi kazi ambacho kilijumuisha Bodi ya Mkonge na Halmashauri ya wilaya ya Korogwe ili kubaini ukweli wa madai ya wakulima.
Bw. Nnyari amesema baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kikosi kazi hicho ni pamoja na kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa kilimo hicho kwa wakulima wadogo na kuagiza Mkaguzi Mkuu wa Heshabu za Serikali kufanya uhakiki wa kubaini uhalali wa madeni yote ambayo kampuni ya Katani inadaiwa na ambayo inawadai wakulima.
“Baada ya uchunguzi huo Serikali ilibaini kwamba Kampuni ya Katani Limited iliwapunja wakulima kuanzia 2008 hadi 2018 jumla ya sh. bilioni 29.4 ambazo ni pamoja na fedha za SACCOS na AMCOS. Aidha wakulima nao walikuwa wanadaiwa kiasi cha sh. bilioni 2.8.”
Amesema Desemba 2018 Serikali ilifanya mabadiliko kwa kuiondoa Kampuni ya Katani Limited katika shughuli za wakulima na kuipa AMCOS kazi ya kusimamia shughuli zote kuanzia utayarishaji wa mashamba, uvunaji na uuzwaji ambao kwa sasa unafanyika kwa kupitia minada na mnunuzi anapatikana kwa njia ya ushindani tofauti na awali ambapo kampuni ya katani ilikuwa mnunuzi pekee.
Mwenyekiti huyo ametaja mafanikio yaliyopatikana baada ya AMCOS kupewa uendeshaji wa mashamba hayo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mapato ya mkulima kutoka sh. 206,000 kwa tani moja hadi kufikia sh. milioni 1.450.
No comments:
Post a Comment