Sunday, March 8, 2020

WANAWAKE RUKWA WATAJIWA WANAOWARUDISHA NYUMA KIMAENDELEO

Baadhi ya Wanawake waliohudhuria Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayofanyika kila tarehe 8 Machi wakipita kwa maandamano huku wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe tofauti mbele ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (hayupo pichani)

Baadhi ya Wanawake waliohudhuria Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika leo, wakipita mbele ya mgeni rasmi wa Maadhimisho hayo Kimkoa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akiuepuka mkono wa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura ikiwa ni njia mojawapo ya kujizoesha tabia ya kutopeana mikono ili kuepukana nanugonjwa hatari unaoenea kwa kasi duniani Covid-19 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatambulisha rasmi wakurugenzi wa halmashauri mbili za mkoa huo wanaochangia kukwamisha maendeleo ya wanawake katika halmashauri zao huku akiwataka wakurugenzi wawili wengine kuhakikisha wanamaliza asilimia nne ya mikopo kwa wanawake kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema kuwa katika halmashauri nne za mkoa huo ni Manispaa ya Sumbawanga pekee ndio inayoongoza kwa utoaji wa mikopo hiyo ikifuatiwa na halmashauri ya Wilaya Kalambo huku halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na halmashauri ya Wilaya ya Sumbanga zikiwa hazina dalili za kufikia lengo hilo hali iliyompelekea Mkuu huyo wa Mkoa kuwasimamisha ili wanawake waliohudhuria kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kuwatambua.
“Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga 4% kati ya 10% inayotakiwa kutolewa kwa wanawake ni shilingi Milioni 86, lakini halmashauri hii imetoa shilingi milioni 10 peke yake, sasa hii haifurahishi walipaswa hadi kufikia sasa kufikia shilingi milioni 45 wawe wamevuka nusu ile inayotakiwa lakini wametoa shilingi milioni 10 tu, kwahiyo mtu anayewaangamiza na anayewadidimiza wanawake katika halmashauri zenu mnaanza kumuelewa mbaya wenu ni halmashauri gani, halmashauri ya Sumbawanga DC hii ndio hali waliyonayo inamaana hawawajali hawa wanawake pamoja na kwamba tunayo sheria inayobana kutekeleza hayo maagizo,” Alisema.
Mh. Wangabo aliongeza kuwa nayo halmashauri ya Nkasi ilitakiwa kutoa shilingi milioni 87 lakini imetoa shilingi milioni 10 tu huku ikisajili vikundi 130 na kuvipa mikopo vikundi 2 vyenye wanufaika 45 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikiwa imesajili vikundi 122 na kutoa mikopo kwa vikundi 3 vyenye wanufaika 63.
“Nitoe rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Rukwa kuhakikisha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2020 fedha zote zilizobaki ziwe zimetolewa vinginevyo watajikuta pabaya na kujikuta wanalia na kusaga meno, huu sio mchezo kwasababu hizi fedha ni za kisheria, kama hutekelezi hii sheria na wakumbuke kuwa huku nyuma kuna madeni ambayo hawakufikia 10% ikiwemo 4% kwa wanawake, 4% kwa vina na 2% kwa watu wenye ulemavu,” Alisema.
Mh. Wangabo aliyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 8 Machi ambapo kimkoa ilifanyika katika viwanja vya Kijiji cha Kisumba, kata ya Kisumba, Wilayani Kalambo akijibu risala iliyosomwa na jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mkoa huo.
Aidha, amewataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanatenga bajeti ya kuyawezesha majukwaa ya wanawake katika halmashauri zao ili kuweza kurahisisha shughuli za majukwaa hayo ambapo katika sherehe hizo aliweza kulizindua jukwaa la wanawake la halmashauri ya wilaya ya Kalambo.
Wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi wa maadhimisho hayo kimkoa Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji kiuchumi Mkoa wa Rukwa Bi.Leonora Jailos alisema kuwa wanawake wa mkoa wa Rukwa wako mstari wa mbele katika shughuli za kilimo na hivyo kujipanga katika kufikia Tanzania ya viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo ikiwemo vya kusindika vyakula na mazao na kueleza kuwa miongoni mwa changamoto wanazopata ni fedha kidogo za mikopo wanazopatiwa na halmashauri.
“Baadhi ya changamoto tulizonazo wanawake wa Mkoa wa Rukwa ni kwamba, moja mikopo ya 4% tunayopewa na halmashauri zetu kwenye vikundi, ni fedha kidogo ambazo hazituendelezi tulivyojipanga ili kutuendeleza kiuchumi, hivyo basi tunaiomba serikali kuangalia namna nyingine kiasi cha fedha kinachotolewa kama mikopo, vile vile wanawake tukopeshwe vifaa kulingana na shughuli za kikundi,” Alisema
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa Mkoa umeendelea kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni kwa kuzindua mkakati wa kimkoa wa kukabiliana na mimba za utotoni kwa lengo la kuhakikisha mtoto wa kike anapata fursa ya kuendelea na masomo yake hadi chou kikuu huku akiwaonya wanaume wenye tabia ya kuwanyanyasa wanawake hasa katika msimu wa mavuno kwa kuuza mazao yote wakati kwenye shughuli za kilimo hakushiriki ipasavyo na matokeo yake hujinufaisha na kuiacha familia katika hali mbaya.
Katika maadhimisho hayo ambayo Manispaa ya Sumbawanga iliweza kung’ara kwa kutokana na rekodi yake ya kutoa shilingi milioni 90 kati ya 165.8 ya 4% ya mikopo kwa wanawake huku ikiwa imesajili vikundi 322 na kutoa mikopo kwa vikundi 138 huku idadi ya wanufaika ikiwa ni wanawake 863 na kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa nay a Baadaye”.

No comments:

Post a Comment