Friday, March 6, 2020

WADAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI KUANZA KUSAKWA NCHI NZIMA

Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew Nhonge akizungumza na Wenyeviti na Watendaji wa Serikali za Mitaa wakati wa uhamasishaji ulipaji kodi ya pango la ardhi mkoa Dodoma leo tarehe 6 Machi 2020. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dodoma Joseph Kamonga na kulia ni Afisa Ardhi Elia Kamyanda.
Baadhi ya Wenyeviti wa Mitaa ya jiji la Dodoma wakimsikiliza Kamishna wa Ardhi Nchini  athaniel Methew Nhonge (hayupo pichani) wakati wa zoezi la uhamasishaji ulipiaji kodi ya pango la ardhi  chini.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dodoma Joseph Kamonga akizungumza wakati wa kuhamasisha zoezi la ukiusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa Wenyeviti na Watendaji wa serikali za Mitaa katika mkoa wa Dodoma leo tarehe 6 Machi 2020. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methewe Nhonge.


Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza operesheni maalum ya kuwasaka wadaiwa wote sugu ya kodi ya pango la ardhi na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kufidia madeni wanayodaiwa.
Akizungumza na Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa katika jiji la Dodoma leo tarehe 6 Machi 2020 Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew Nhonge alisema opresheni hiyo inaanza leo kwa nchi nzima ambapo wamiliki wote waliopelekewa ilani za madai wanatakiwa kulipa madeni yao kufikia Machi 9, 2020.
Alisema, wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ambao hawajapelekewa ilani hadi kufikia leo tarehe 6 Machi 2020 watatakiwa kukamilisha kulipa kodi hiyo April Mosi 2020 na watakaokaidi watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na mali zao kunadiwa kufidia deni.
‘’ Kuna madhara makubwa usipolipa kodi, pale itakaposhindikana mtu kulipa kwa kufuata taratibu basi hatua za kumfikisha mdaiwa mahakamani zitafanyika na huko hatuangalii bei ya soko bali tunatafuta kodi yetu tu’’ alisema Nhonge.
Aidha, alibainisha kuwa, katika maeneo mbalimbali kuna viwanja vimepimwa lakini wamiliki wake wameshindwa kuchukua hati kwa kuhofia kulipa kodi ya pango la ardhi ambapo aliwataka wamiliki hao kwenda ofisi husika kuchukua hati ili kuwa na umiliki haali.
Kwa mujibu wa Nhonge, lengo la wizara yake ni kukusanya takriban bilioni 180 katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2019/2020 na moja ya mkakati wa kufanikisha lengo hilo ni kuhirikisha wenyeviti wa mitaa kutokana na ukaribu wao kwa wananchi.
Alisema, Wizara imeanisha takriban vituo 185 kwenye Halmashauri za Wilaya, Majiji na Manispaa na kusisitiza vituo hivyo vitakuwa vikifanya kazi hadi siku za jumamosi ili kuwapa nafasi wamiliki wa ardhi kulipa kodi hiyo.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dodoma Joseph Kamonga aliwataka Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa katika jiji la Dodoma kuisaidia Wizara ya Ardhi kuelimisha  wananchui umuhimu wa kulipa kodi ya ardhi na kubainisha kuwa elimu hiyo itakapowaingia itasaidia kuongeza makusanyo kwa serikali.
Baadhi ya wenyeviti wa mitaa katika jiji la Dodoma waliitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwapatia ramani za mitaa yao kwa maelezo kuwa baadhi ya maeneo yao  wamiliki wake wamekuwa hawajulikani.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Ilazo Mbuyuni Lucas Fredy aliitaka Wizara kuongeza kasi ya utoaji Hati pamoja na Vibali vya ujenzi  ili kuharakisha maendeleo na kuongeza kuwa utunzaji mbovu wa majalada ya ardhi nao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji utoaji hati.

No comments:

Post a Comment