Sunday, March 8, 2020

Tunapaswa kujivunia kwa kuongeza eneo la uzalishaji wa mbegu, miche bora pamoja usajili wa Wakulima na watoa huduma za kilimo – Waziri Hasunga

Afisa Mawasiliano serikalini Wizara ya Kilimo Ndg Issa Sabuni (Mwenye Fulana) jambo mbele ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mwenye Tai) wakati wa uzinduzi wa mtandao wa kutoa habari (Kilimo Tv) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano maarufu Kilimo IV Jijini Dodoma tarehe 8 Machi 2020. Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya (asiye na Tai) na  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo (Mwenye kaunda suti). (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akifuatilia mkutano wa Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma Tarehe 8 Machi 2020. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya wakifuatilia kwa makini mkutano wa Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma Tarehe 8 Machi 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wenyeviti wa Bodi za mazao mara baada ya kumalizika mkutano wa Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma Tarehe 8 Machi 2020.

Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema Watendaji wa Wizara ya Kilimo anayoiongoza wanapaswa kujivunia kwa mafanikio mengi waliyoyapata chini ya uongozi wake.

Ameyasema hayo mapema leo, tarehe 8 Machi 2020 wakati akifunga mkutano wa kikazi, mkutano uliowajumuisha Wenyeviti, Wakuu wa Bodi za Mazao, Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.

Waziri Hasunga amesema Wizara ilifanikiwa kusajili Wakulima wa mazao ya kimkakati na yanasimamiwa na Bodi za Mazao; mazao hayo ni pamoja na chai, kahawa, korosho, sukari, pamba, mkonge, tumbaku na pareto.

“Najivunia kuanzisha mfumo wa usajili wa Wakulima wa mazao nane ili kuwa na kanzidata ya Wakulima wa mazao hayo yenye kusimamiwa kupitia Bodi za Mazao na baada ya zoezi hili kukamilika; tutaanza kuwasijili Wakulima wa mazao mengine, na sambamba na hili tumeanza kuwasajili Wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo.” Amekaririwa Waziri Hasunga.

“Kwa ujumla tumefanya vizuri kwa kuvuka lengo la usajili wa Wakulima kwani tumesajili Wakulima 1,279,884 kati ya Wakulima 1,377,069 na tunataraji kuanza kuwapa vitambulisho ili na wao watambulike kama Watumishi wengine katika kada mbalimbali wanavyotambuliwa.” Amesisitiza Waziri Hasunga

Waziri ametaja mafanikio mengine ni pamoja na Wizara kuanza kutoa vibali mbalimbali vya mazao ya kilimo kwa mfumo wa Kielektroniki (ATIMS), mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa eneo la uzalishaji wa mbegu bora, kutoka hekta 10,887 mwaka 2015/2016 hadi 94,368 2018/2019 ambapo uzalishaji umetoka tani 10,000 hadi tani 71,207

Waziri Hasunga ameongeza kuwa uzalishaji wa miche na vipando bora vya mazao ya kilimo umeongezeka kutoka miche milioni 5 mwaka 2015/2016 hadi miche na vipando milioni 22,707,000

Waziri Hasunga amesisitiza kuwa Watendaji wa Wizara wanapaswa kuongeza juhudu katika masuala ya mikakati, programu na usimamizi kwa Maafisa Ugani ili uzalishaji uongezeke kwenye mazao ya kimkakati kama pamba, kahawa, tumbaku na chai.

Katika kulitekeleza hilo Waziri Hasunga amemuagiza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kuhakikisha anaanda malengo ya kuongeza uzalishaji kwa mazao yote kwa mwaka ujao wa 2020/2021.

MWISHO

No comments:

Post a Comment