Meneja wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Dodoma Happiness Kizigira akimpatia zawadi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipomtembelea ofisini kwake eneo la Mtumba jijini Dodoma jana kwa lengo la kubadilishana mawazo ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kulia ni Afisa Mahusiano wa benki hiyo Neema Malisa na Afisa Masoko Silvia Mokiria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipeana mkono na Afisa Mahusiano wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Neema Malisa baada ya kutembelewa na ujumbe wa Benki hiyo jana ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma. Kushoto ni Meneja wa NBC tawi la Dodoma Happiness Kizigira na wa pili kulia ni Afisa Masoko Silvia Mokiria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Dodoma walipomtembelea ofisini kwake eneo la Mtumba jijini Dodoma. Kushoto ni Meneja wa Benki hiyo Hapiness Kizigira. Kulia ni Afisa Uhusiano Neema Malisa na wa pili kulia ni Afisa Masoko wa benki hiyo Silvia Mokiria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipongeza Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kuanzisha utaratibu wa kutembelea viongozi wanawake kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusiana na uboreshaji huduma za benki hiyo.
Dkt Mabula alitoa pongezi hizo jana ofisini kwake jijini Dodoma baada ya kutembelewa na ujumbe wa NBC ukiiongozwa na Meneja wa Tawi la Benki hiyo jijini humo Bi. Happiness Kizigira ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Alisema, utaratibu ulioanzishwa na Benki ya Taifa ya Bisahara (NBC) kwa kutumia maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kutembelea viongozi wanawake kwenye maeneo tofauti nchini ni mzuri na wa kipekee unaotoa fursa kwa benki hiyo kubadilishana mawazo kupitia viongozi hao kwa lengo la kuboresha huduma zake.
‘’Kwanza nashukuru sana kwa kumfuata mwanamke pale mahali alipo, aina hii inavutia na inatoa muda wa kubadilishana mawazo, iko very unique badala ya kwenda viwanjani. Alisema Dkt Mabula.
Aliueleza ujumbe huo wa NBC tawi la Dodoma kuwa, pamoja na benki hiyo kutumia fursa hiyo kuelezea shughuli zake lakini inatoa nafasi pia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wateja wake kupitia wanawake kutokana na kuwa na nafasi kubwa kuufikisha ujumbe kwa wananchi wengi.
Kwa upande wake Meneja wa NBC tawi la Dodoma Bi.Happiness Kizigira alisema, benki yake imeanzisha utaratibu wa kuwatembelea viongozi wanawake kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ili kutoa shukurani sambamba na kuthamini mchango wa wanawake katika shughuli za ujenzi wa taifa.
Kwa mujibu wa Kizigira, wanawake ni jeshi kubwa linalohitaji kuungwa mkono ndiyo maana benki yake imeamua kuwatumia kufikisha ujumbe wa namna bora ya kutunza fedha kupitia Benki ya Taifa ya Biashara.
Meneja huyo wa NBC tawi la Dodoma aliongeza kuwa, benki yake inahamasisha wanawake kutunza fedha kupitia benki hiyo ili kujikwamua kiuchumi na kubainisha kuwa kwa sasa NBC ina huduma nyingi ikiwemo mikopo ya riba nafuu sambamba na ufunguaji akaunti wa haraka unaojulikana kama ‘Faster Acc’ alioueleza kuwa unamuwezesha mteja kufungua akaunti ndani ya muda mfupi.
No comments:
Post a Comment