Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kahawa Bwana Kajiru Kisenge kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Kahawa akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima kulia kwa Mkuu wa mkoamni Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Bi. Karoline Albert Mthapula, leo tarehe 10 Machi 2020.
Adam Malima Mkuu wa mkoa wa Mara akiwa ameshika moja ya mche bora wa kahawa aina ya arabika pembeni yake kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Antony Mavunde wengine kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Albert Mthapula, mwenye suti ya bluu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Kahawa, Profesa Jamal Adam na kulia kwa Katibu Tawala ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kahawa Bwana Kajiru Kisenge, leo tarehe 10 Machi 2020.
Adam Malima Mkuu wa mkoa wa Mara akitoa maelezo baada ya kukabidhiwa sehemu ya miche 40,000 ya kahawa aina ya arabika pembeni yake kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) Antony Mavunde wengine kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Albert Mthapula, mwenye suti ya bluu Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Kahawa Profesa Jamal Adam na kulia kwa Katibu Tawala ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kahawa Bwana Kajiru Kisenge, leo tarehe 10 Machi 2020.
Sehemu ya kitalu cha miche bora ya kahawa aina ya arabika 40,000 iliyokabidhiwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Kahwa, Profesa Jamal Adam kwa Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima, leo tarehe 10 Machi 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima ameipongeza Bodi ya Kahawa kwa kutimiza ahadi yake ya kuupa mkoa wake miche bora ya kahawa aina ya arabika mbapo jumla ya miche 40,000 imekabidhiwa katika hafla fupi iliyofanyika leo, tarehe 10 Machi, 2020 katika Ofisi ya Mkuu wa
mkoa wa Mara, Mjini Musoma.
Akiongea wakati wa hafla hiyo, Mhe. Adam Malima amesema Bodi ya Kahawa imeonyesha kwa vitendo dhamira yake kama msimamizi wa sekta ndogo ya zao la kahawa kwa kutoa miche 40,000 bora ambayo itasambazwa katika wilaya za mkoa wa Mara ili kuwapa bure, Wakulima ambao wengi wamejiandaa kuipokea na kuipanda.
Mhe. Malima amesema azimo la kuongeza uzalishaji na tija lilifikiwa na Wadau wa zao la kahawa, katika mkutano wa Kamati Ndogo, uliofanyika Mjini Moshi na kukubaliana kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Kahawa kuanza mapinduzi ya kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa kutoka tani 50,000 za sasa hadi tani 200,000 ifikapo mwaka 2023.
“Kwenye mkutano wetu wa kamati ndogo ya kahawa, tuliokutana Mjini Moshi, mwezi mmoja uliopita, tulikubaliana kwa pamoja kuongeza uzalishaji na sioni sababu kwa nini tusiizidi nchi ya Uganda ambayo ina eneo dogo lakini inazalisha zaidi ya tani 295,000.” Amekaririwa Mkuu wa
mkoa wa Mara.
Mhe Malima amesema Serikali ya mkoa imewaanda Wakulima wake na tayari vitalu vimeandaliwa ili kuhakikisha kuwa Wakulima katika wilaya ya Tarime na wilaya zote za mkoa, wanaongeza uzalishaji kwa kupanda miche hiyo.
“Tumeshaanda mkakati wa mkoa, tumegawana majukumu na niseme tu kuwa Tarime inafanya vizuri na inaongoza ukilinganisha na wilaya ya Butiama, Serengeti na Rolya; tumeshaanzisha vitalu katika wilaya hizo, bila shaka tutaongeza uzalishaji kutoka 15,000 kimkoa za sasa na kufanya vizuri zaidi”. Amesisitiza Mhe Malima.
Akiongea baada ya kukabidhi miche hiyo, Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Kahawa, Profesa Jamal Adam amemshukuru Mkuu wa mkoa wa Mara kwa namna ambavyo amedhamilia kuongeza tija na uzalishaji kwenye mkoa wa Mara na ameahidi kuwa Bodi ya Kahawa itaongeza miche 60,000 zaidi ambayo, itapandwa kwenye shamba kubwa la Jeshi la Magereza, Mjini Tarime.
Profesa Jamal Adam ameongeza kuwa Bodi ya Kahawa imeanzisha mkakati wa pamoja wa kuongeza eneo la kilimo cha kahawa kwa kuwahamasisha Wakuu wa mikoa inayolima kahawa na kwa kuanzia
uhamasishaji unalenga kila mkoa wilaya inayolima kahawa kuanzisha mashamba mashamba mawili makubwa ya kahawa na kwa kufanya hivyo, uzalishaji utaongezeka katika kipindi kifupi.
“Tuna mashamba makubwa 101 nchini kote, tumekubaliana ili kuongeza uzalishaji wa sasa ambao ni tani 50,000 ni kwa kila wilaya kuanzisha mashamba mawili makubwa ambapo Bodi ya Kahawa, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zitashirikiana na Serikali za mikoa kuhakikisha mashamba hayo yanakuwa endelevu, kwa kufanya hiyo tutafikia uzalishaji wa tani 200,000 katika kipindi kifupi”. Amesisitiza Profesa Jamal Adam.
Kaimu Mkurugenzi Bodi ya Kahawa ameongeza kuwa Bodi ya Kahawa itaanzisha mkakati wa kuhamasisha kilimo cha kahawa kuanzia kwenye shule za msingi na sekondari na kwa kufanya hiyo, watoto watajengewa mazingira ya kuanza kulipenda zao la kahawa tangu wakiwa wadogo.
“Tumeanda mkakati wa kuhamasisha kilimo cha zao la kahawa kuanzia kwenye shule za msingi na sekondari kwenye maeneo yaliyolima kahawa, shule za msingi na sekondari ziwe na mashamba ya kahawa, jambo hili litaongeza uzalishaji; ninaamini ndani ya kipindi kifupi, uzalishaji, utaongezeka na kufikia tani 200,000. Amesisitiza Profesa Jamal.
Profesa Jamal ameongeza kuwa Bodi ya Kahawa ipo kwenye maboresho makubwa na kudokeza kuwa kwa sasa imeanda mkakati mwengine wa kuwasaidia Wakulima wadogo wa zao la kahawa nchi kuongeza matumizi ya mbolea, ambapo ameeleza kuwa Mkulima wa Tanzania anatumia kilo 7 za mbolea kwenye hekta moja; matumizi hayo ni ya chini sana ukilinganisha na nchi ya Vietnam na Brazil ambapo Mkulima anatumia zaidi ya kilo 143 hadi 310 kwa hekta.
No comments:
Post a Comment