Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na watendaji wa Jeshi mara baada ya kukagua mradi wa Ujenzi wa wodi ya wazazi unaendela katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake Mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Uzalishaji mali la JKT(SUMA JKT).
Meneja wa SUMA JKT Kanda ya Ziwa Kapteni Fabian Buberwa akiwaongoza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge(wa nne kushoto) kuelekea katika eneo la ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi, wakati wa ziara Mkuu huyo wa JKT Mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT.
Katibu Tawala Msaidizi seksheni ya Miundombinu katika Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mashaka Luhamba akitoa maelezo ya hali ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT Mkoani Simiyu kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Brigedia Jenerali Charles Mbuge , wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa JKT Mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa pili kushoto) akizungumza jambo katika ziara ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) Brigedia Jenerali Charles Mbuge Mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) Brigedia Jenerali Charles Mbuge(kulia) akimkabidhi kalenda Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akiwa katika zaira ya kikazi mkoani humo Februari 13, 2020 yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na SUMA JKT.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Brigedia Jenerali
Charles Mbuge amesema kuwa baadhi ya wazabuni wanaouza vifaa vya ujenzi
wamekuwa wakiuza vifaa kwa bei ya juu na kuchelewesha vifaa hivyo pale
vinapohitajika, jambo linalopelekea baadhi ya miradi inayotekelezwa na Shirika
laUzalishaji Mali la Jeshi hilo (SUMA JKT) kutokamilika kwa wakati.
Brigedia Jenerali Mbuge ameyasema hayo Februari 13, 2020 mjini
Bariadi wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na
SUMA JKT mkoani Simiyu.
Ameongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) limejipanga kuanzisha maduka ya vifaa vya Ujenzi
vitakavyouzwa kwa bei ya jumla ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa kwa
urahisi, haraka na kwa bei nafuu ikilinganishwa na wazabuni wengine.
“Tatizo moja ninaloliona kwenye utekelezaji wa miradi ni vifaa
kuuzwa kwa bei ya juu sana na kucheleweshwa, tumeamua kuwa na maduka ya
vifaa ya jumla; tutatoa maelekezo kwa wakuu wa kanda za ujenzi watatupatia
mahitaji yao, ili kuwawezesha kufanya kazi kwa wakati kama tunavyokubaliana na
washitiri wetu,” alisema Brigedia Jenerali Mbuge.
Katika hatua nyingine Brigedia Jenerali Mbuge amesema jeshi hilo
litaendelea kuwatumia vijana watakaomaliza mafunzo ya JKT katika shughuli zilizopo
kwenye miradi inayotekelezwa na Jeshi hilo lengo likiwa kuwawezesha vijana hao
kupata kipato na baadaye waweze kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.
Vile vile ameahidi kuongeza nguvu kazi ya vijana katika mradi
inayotekelezwa na SUMA JKT mkoani Simiyu kuongeza kasi na miradi hiyo iweze
kukamilika kwa muda uliopangwa, huku akitoa wito kwa Taasisi mbalimbali kuipa
kazi SUMA JKT, ili iendelee kuwa kutoa gawio kubwa kwa Serikali, ambapo
amesema mwaka 2018/2019 ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja na mwaka
2019/2020 linatarajia kupanda zaidi kutokana na uwepo wa vyanzo vya kutosha.
Awali akitoa taarifa, Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya
miundombinu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mhandisi Mashaka
Luhamba amesema JKT wanatekeleza miradi minne mkoani Simiyu ukiwemo wa
ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wodi ya wazazi Hospitali ya
Rufaa ya mkoa, ujenzi jengo la wizara ya kilimo linalojengwa kwenye
viwanja vya maonesho ya Nane nane pamoja na kiwanda cha Chaki Maswa (
Maswa chalk) .
Aidha mhandisi huyo amebainisha kuwa ujenzi wa jengo la Mkuu wa
Mkoa unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya shilingi bilioni
5.7 ambapo ujenzi rasmi ulianza mwezi Mei, 2019 na endapo fedha
zitapatikana kwa wakati unatarajiwa kukamilika Novemba, 2020.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema
ni vema SUMA JKT ikahuisha uharaka wa kutekeleza miradi kama jamii
inavyoutarajia kwa kuwa jamii na Serikali imejenga imani kubwa kwa JKT
kutekeleza miradi kwa wakati ikilinganishwa na wakandarasi wengine.
Mtaka ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa na SUMA JKT iwe fursa
kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT na kumaliza mikataba yao ili waweze kupata
kipato kitakachowasaidia kwenda kujitegemea na kujiajiri endapo hawataajiriwa.
No comments:
Post a Comment