Kaimu Naibu Mraijis wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde
Warajis Wasaidizi wa Vyama
vya Ushirika wa Mikoa wametakiwa kuwashirikisha Viongozi wa Vyombo vya Usalama
katika ngazi ya wilaya kwenye hatua ya upekeuzi wa Wanachama wanaoomba kugombea
uongozi katika Vyama vya Ushirika ili kupata viongozi wenye sifa.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu
Naibu Mraijis wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde kwa Waandishi wa
Habari leo, Ijumaa Januari 31, 2020 Jijini Dodoma amewataka pia Warajis
Wasaidizi kuhakikisha kuwa wanachama wote wa Vyama vya Ushirika wanapata fursa
ya kuchukua fomu za kugombea uongozi katika vyama vyao.
“Warajis Wasaididizi na Maafisa
Ushirika walioko katika ngazi za wilaya wahakikishe kuwa viongozi wa Vyombo vya
Usalama katika ngazi ya wilaya wanashirikishwa katika hatua ya upekeuzi.
Ushirikiano huu utatusaidia kuwapata viongozi waaminifu na waadilifu. Viongozi
walioko katika ngazi za vijiji na Kata nao wana mchango mkubwa katika kuwapata
viongozi wenye sifa zinazotakiwa; hivyo nao washirikishwe katika zoezi la
upekuzi,” amesema Bw. Malunde.
Kaimu Naibu Mraijis wa Vyama
vya Ushirika, Bw. Malunde amesema kuwa Mwaka huu 2020 ni mwaka wa uchaguzi katika
Vyama vya Ushirika na ametoa rai kwa wanachama kuhakikisha kuwa viongozi
wanaowachagua ni wale walio na sifa stahiki watakaowezesha kulinda na
kuendeleza mali na maslahi ya Wanaushirika.
“Katika kuhakikisha kuwa Vyama
vya Ushirika vinapata viongozi ambao watakuwa na mchango mkubwa katika
maendeleo ya ushirika nchini, hatuna budi kushirikiana sote katika kuwapata
viongozi hao,” amesema Bw. Malunde.
Kuchaguliwa kwa viongozi
wasiokuwa waaminifu na waadilifu katika Vyama vya Ushirika kunasababisha mali
za Wanaushirika kuibiwa na viongozi hao na hatimaye vyama hivyo kufilisika.
Mwanachama wa kawaida anaweza kuilaum Serikali, bila kujua kuwa viongozi
wanaoiba mali za chama chake aliwachagua yeye mwenyewe.
Bw. Malunde amesema kuwa katika
tukio la hivi karibuni mkoani Njombe, Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa
Hussein Bashe, alitoa maagizo ya urejeshaji mali za ushirika zilizokuwa zimeporwa
na Viongozi wasio waaminifu wa Ushirika wa eneo la Lupembe mkoani humo.
Kutokana
na maelekekezo ya Serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na
Vyombo vya Dola wamefanikiwa kurejesha mali mbalimbali za wanaushirika
zilizokuwa zimechukuliwa na wajanja wachache kwa kushirikiana na Viongozi wa
Ushirika wa eneo hilo.
Mali zilizopatikana ni pamoja na magari sita
(6): Mitsubish Canter - 3, Toyota land cruiser – 1, Escudo – 1 na Rock – 1;
Injini za magari – 2; Jenereta – 1; Mashine nne za kuvunia chai; Shamba moja la
chai lenye ukubwa wa hekari 215 na Nyumba moja ambayo iko jirani na shamba la
chai la ekari 215 katika kitongoji cha Mbingu kata ya Lupembe.
Zoezi la kuhakikisha
urejeshaji wa mali za wanaushirika wa Njombe pamoja na mali za vyama vya
ushirika vingine bado linaendelea ili kuhakikisha mali zote za Vyama vya
Ushirika zinarejeshwa na kuwekwa katika mikono salama.
“Huu ni mfano dhahiri kuwa tusipokuwa na
viongozi waaminifu na waadilifu hakika juhudi za kufufua na kuimarisha ushirika
hazitazaa matunda yoyote. Ni imani yangu kuwa kila mdau akisimamia sehemu yake
husika na kuisimamia kwa uaminifu tutarejesha heshima ya ushirika iliyopotea
kwa muda sasa. Wanachama wa vyama vya ushirika wana mchango mkubwa katika
kufanikisha hili,” amesema Kaimu Naibu Mraijis wa Vyama vya Ushirika.
No comments:
Post a Comment