Sunday, February 23, 2020

WAFANYABIASHARA IRINGA WAFURAHIA KAMPENI YA ELIMU KWA MLIPAKODI

 Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Ernesta Shirima akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la jumla na rejareja wa Manispaa ya Iringa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo.
 Meneja Utawala wa Kampuni ya Ever Green Wood Bw. Edward Wong iliyopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwaonyesha Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakikagua Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) cha Kampuni ya Ever Green Wood iliyopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo.
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa wameifurahia kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo na kuiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kampeni hiyo mara kwa mara ili waweze kuelewa kwa undani zaidi masuala mbalimbali yanayohusu kodi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni hiyo, wafanyabiashara hao wamesema kuwa, wamefurahishwa na kitendo cha TRA kuwafikishia elimu ya kodi sehemu wanazofanyia biashara kwani imekuwa rahisi kwao kueleza changamoto zao na kuelimishwa mambo ya kodi ambayo mengine hawakuwa na uelewa nayo.
“Binafsi nimefurahi kutembelewa na TRA kazini kwangu hapa na kutokana na elimu niliyopewa na maafisa wa TRA, nimetambua kwamba kuna mambo niliyokuwa nayafanya kwa kutokuwa na elimu tu, mfano mzuri ni utunzaji wa kumbukumbu za biashara yangu, leo nimejifunza umuhimu wake na ninaanza kufanya hivyo mara moja,” alisema Vitusi Muhungile ambaye ni mfanyabiashara wa duka la vipodozi mkoani humo.
Naye, Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wa Manispaa ya Iringa, Samson Ngakonda, alisema kwamba, elimu ya kodi ina umuhimu sana kwani baadhi ya wafanyabishara elimu yao ni ya chini hivyo kutembelewa na TRA kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kodi ni msaada mkubwa kwao.
“Elimu tuliyopewa leo ina umuhimu mno maana unaweza kukosea na ukipata elimu ukabadilika hivyo ninaomba elimu hii ifanyike mara kwa mara ili hata sisi ambao hatukwenda shule tuweze kujua vizuri haya mambo ya kodi,” alisema Ngakonda.
Kwa upande wake Dinna Mwampendwa ambaye ni mfanyabiashara wa mbao katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa amesema kuwa, kutokana na elimu ya umuhimu wa kutumia Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti (EFD) aliyopata kwenye kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea wilayani humo, ameamua kuanza kufuatilia mashine hiyo ili aweze kuinunua. 
“Leo nimejisikia vizuri kutembelewa na maafisa wa TRA kwenye biashara yangu, mwanzoni nilivyoona gari niliogopa lakini baadae nikaona wamekuja kirafiki na wamenielimisha mambo mengi na hasa umuhimu wa kutumia mashine ya EFD na kuanzia leo naanza kuwatafuta mawakala ili ninunue mashine na mimi,” alieleza mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara mwingine aliyefurahia kampeni ya elimu kwa mlipakodi na kuamua kuungana na Bi. Mwampendwa kufuatilia mashine ya EFD ni Kassim Urassa anayefanya biashara ya kusafirisha mbao ambaye amesema kuwa, elimu aliyoipata hajawahi kuipata popote hivyo ameamua kufuatilia mashine hiyo kwa sababu anastahili kuwa nayo.
“Sijawahi kubahatika kupata elimu hii kwa sababu ya shughuli zangu za kusafiri mara kwa mara. Kwakweli nimeelewa vya kutosha na ninaomba kiwekwe chumba maalumu katika ofisi za TRA ili kabla mfanyabiashara hajaanza biashara, aweze kuelimishwa kwa undani kuhusu kodi kwa lengo la kuepuka kufanya makosa,” alisema Urassa.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inaendelea kufanyika mkoani Iringa na kwa sasa timu ya maafisa wa TRA wanaofanya kampeni hiyo wako wilayani Mufindi baada ya kutoka Wilaya ya Kilolo na Manispaa ya Iringa.

No comments:

Post a Comment