Na Innocent Natai (TPRI)
Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (Tropical Pesticides Research Institute (TPRI) hivi leo imesaini mkataba na kampuni ya mawasiliano ya TTCL utakao wawezesha wakulima kugundua viuatilifu wanavyo tumia kuwa ni halisi au bandia kwa kutumia simu ya mkononi.
Mkataba huo umesainiwa hivi leo makao makuu ya Kampuni ya Mawasiliano ya TTCL,baina ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu katika Ukanda wa Kitropiki (Tropical Pesticides Research Institute (TPRI) Dkt. Margaret Mollel na Kaimu mkurugenzi mkuu wa Tanzania Telecommunications Company Ltd (TTCL) Bi Kezia Katamboina,mbele ya baadhi ya watendaji wa TTCL na TPRI akiwemo Kaimu Msajili Mkuu wa Viuatilifu Nchini Joseph Bukalasa.
Katika mpango huo Mkulima ataweza kutambua kiuatilifu alichonunua kwa kutumia hata simu ya tochi na haina ulazima wa kutumia simu ya kisasa yaani Smart Phone.
Akieleza katika makubalianao hayo Kaimu Mkurugenzi Kezia Katamboina amesema TTCL imeadhimia kuondoa kero kwa wakulima kwa kuweka mawasiliaano yatakayo wawezesha mkulima kujinasua kutoka kwa wafanyabiashara wasiowaadilifu wanaofifisha juhudi za serikali kwa kuwauzia na kusambaza viuatilifu visivyo na ubora au ambavyo havija kaguliwa na kusajiliwa na TPRI hivyo mfumo huo utaweza kuwasaidia wakulima kikamilifu kuepuka kupata hasara kwa kuuziwa viuatilifu hivyo.
Na kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPRI Dkt. Margaret Mollel amesema kuwa mpango huu unaojulikana kama T HAKIKI utakuwa ni mwarobaini wa kukomesha, kusambaa kwa Viuatilifu visivyo na sifa hapa nchini ikiwemo Visivyo kaguliwa na kusajiliwa,Vilivyoisha muda wa matumizi na Visivyo na ubora.
Aidha Dkt. Margaret Mollel ameongeza kuwa baada ya kuhakiki mkulima atakapoona tofauti kwenye kiuatilifu alichonunua kuna namba ataitumia kutoa taarifa TPRI na wataalam wa Taasisi wataweza kujua mahali alipo mkulima na kuweza kumfikia mahali alipo kuangalia tatizo lake na kulipatia Ufumbuzi.
Amemaliza kwa kusema kuwa kupitia mapango huo TPRI haitakuwa na uvumilivu kwa wafanyabiahsara watakaogundulika kuhujumu wakulima kwani kila atakaefanya udanganyifu atagundulika mara moja kupitia mtandao wa simu za TTCL
Taasisi ya TPRI ni taasisi ya Umma iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo ikiwa na majukumu ya Kufanya utafiti, kutathmini na kusambaza matokeo yanayohusu matumizi ya viuatilifu na tabia zake katika kudhibiti visumbufu vya nchi za Ukanda wa Kitropiki kwa kutumia njia za angani na ardhini; kudhibiti visumbufu vya kilimo, magonjwa ya mimea, ndege waharibifu, panya, ndorobo, mbu, konokono, kupe, madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu, kemia ya viuatilifu, fizikia ya viuatilifu, uhandisi wa mabomba, sayansi ya mimea pamoja na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment