Wednesday, February 19, 2020

SPIKA NDUGAI AZINDUA PROGRAMU YA KULIOMBEA TAIFA, ATOA WITO



Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala akimkabidhi kwa niaba ya Spika Ndugai, mkewe Dkt.Fatma Mganga ambaye alimwakilisha Spika katika uzinduzi wa Programu ya Kuliombea Taifa zawadi ya saa zenye picha na ujumbe maalum wa Mungu kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli na Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, baada ya uzinduzi uliofanyika katika Chuo cha Mipango ukumbi wa Mwalimu Nyerere. (Na Mpiga Picha Wetu).

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka watumishi wa Mungu nchini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake ili Mungu azidi kuwapa moyo wa uzalendo,uadilifu kama alivyoonyesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli hatua ambayo inawezesha Taifa kustawi kiuchumi kila kona.


Akizungumza kwa niaba ya Spika Ndugai, mkewe Dkt.Fatma Mganga wakati wa maombi maalum ya kuliombea Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli kuelekea Uchaguzi Mkuu alisema, kila mmoja wetu anapaswa kuliombea Taifa letu, kwani kila penye mafanikio huwa maadui wanainuka, lakini kwa uweza wa Mungu hakuna lisilowezekana.



Mbali na hayo Dkt.Mganga kwa niaba ya Spika Ndugai ambaye alikuwa mgeni rasmi alizindua rasmi Programu ya Kuliombea Taifa inayoratibiwa na Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania katika Chuo cha Mipango ndani ya Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dodoma huku akisisitiza huo ni mkakati mwema kwa ajili ya kulikabidhi Taifa kwa Mungu ili lizidi kuwa lenye mafanikio na baraka tele.



"Taifa kama Taifa halina dini, lakini Taifa haliwezi kuitwa Taifa kama halina watu, lakini watu wake wana dini, kuna dini ya Wakristo, Waislamu na nyingine nyingi, lakini madhehebu yote hayo au imani zote zinatambua kwamba Mungu yupo. Niseme kuwa, nimeyasikia maelezo ya Nabii Joshua kuhusu safari ya nchi nzima kuiombea nchi yetu.



"Hii ni kazi nzito sana, hii ni kazi nzito sana ambayo ninaamini ni kwa uweza wa Mungu tu anaweza kufanya kazi hiyo, lakini ninaamini kwa imani na kwa ushirikiano wetu na wa watumishi wa Mungu atafanikisha kazi hiyo, kwani ninaamini kuwa mwaka 2020 ni mwaka wa kuinuliwa, hivyo mwaka huu tunaenda kuwa Taifa lenye ushindi mkubwa.



"Kwa maombi hayo nchi yetu itaendelea kuwa na amani na itaendelea kubarikiwa, maana huu ni mwaka wa kuinuliwa na hasa ikizingatiwa viuongozi wetu wakiongozwa na Rais wetu mpendwa (Dkt.John Magufuli) wanachapa kazi kwa bidii,Mungu aendelee kuwabariki watumishi wa Mungu na hasa Nabii Joshua, Nabii Joshua ni tuzo, tunaweza kujiuliza tuzo ni nini, tuzo ni zawadi, zawadi inaweza kuwa zawadi bora kama ni zawadi ya kiroho, mimi ninaamini na kwa kupitia kazi na makongamano yake mengi ambayo amekuwa akiyafanya hakika huyu ni mtumishi wa Mungu mwenye kipawa cha kipekee,"alifafanua Dkt.Mganga kwa niaba ya mumewe.



Alisema, yeye kwa niaba ya Spika Ndugai na Serikali wataendelea kuunga mkono juhudi kama hizo ambazo zinaongozwa na Nabii Joshua kwa ajili ya kuliombea Taifa, kuwaunganisha Watanzania na kuwahubiria habari njema kupitia neno la Mungu.



Pia alisema,Nabii Joshua, Mungu amemkirimia kipawa maalum ambacho anaamini wasaidizi wake wakiendelea kumsaidia na kumuombea ili aweze kuyatimiza maono yake kwa ajili ya Taifa letu, Taifa litasonga mbele na Watanzania watazidi kumtumikia Mungu.



"Mungu azidi kuibariki huduma yenu hii, kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni mume wangu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nikiwa nimemuwakilisha ninawaomba watanzania wenzangu tuendelee kuliombea Taifa letu na viongozi wake, kwani kwa Mungu hakuna lisilowezekana," alisema.



Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania (Haki Ministry), Nabii Joshua Aram Mwantyala ambaye pia ni mwasisi wa Programu ya Kuliombea Taifa (Pray for Nation) alisema kuwa, maombi hayo yatafanyika nchi nzima kwa ajili ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wasaidizi wake na Watanzania kwa ujumla.



"Ndugu mgeni rasmi, kuifikia mikoa yote nchini tunatakiwa tuwe na bajeti ya zaidi ya shilingi milioni 300, fedha ambazo ni nyingi, lakini tunaamini kwa michango yenu na maombi yenu hiyo bajeti ni ndogo na Mungu atafanikisha yote ili programu hii ya Kitaifa iweze kuwa na mafanikio zaidi,"alisema Nabii Joshua.



Nabii Joshua alifafanua kuwa, wito huo wa kuliombea Taifa ni kwa Watanzania wote, hivyo bila kujali imani, kabila au rangi kila mmoja atashiriki kwa ajili ya kumlilia Mungu ili azidi kulitendea mema Taifa letu.



“Kwa sababu tulimlilia akatupatia kiongozi na Rais Dkt.Magufuli ambaye anatutetea wanyonge na kuzipigania rasilimali zetu ili ziweze kutumika katika uwiano sahihi kwa maslahi ya Watanzania wote, vivyo hivyo tunapaswa kumuombea Rais wetu ili kwa kushirikiana na wasaidizi wake wazidi kuliletea Taifa letu heshima kubwa, hakika Mungu ameweka kusudi ndani yao kwa maslahi ya Taifa, tunaamini yote yanawezekana,”alifafanua Nabii Joshua.



Kiongozi huyo alisema, katika maombi hayo watamuomba Mungu azidi kuibariki miradi yote iliyopo nchini ikiwemo ya kimkakati kuanzia barabara, reli, viwanja vya ndege, elimu, afya, nishati, mipango ya kudumisha amani na upendo, uchaguzi ujao na mingine mingi.



Baada ya uzinduzi wa Programu hiyo, Nabii Joshua alimzawadia Rais Dkt. Magufuli na Spika Ndugai zawadi ya saa zenye picha zao na ujumbe wa neno la Mungu ambapo zawadi hizo zilipokelewa na mke wa Spika Ndugai, Dkt. Fatma Mganga wakati wa maombi maalum ya kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu.



Nabii Joshua alisema baada ya uzinduzi huo jijini Dodoma, Programu ya Kuliombea Taifa itaelekea mkoani Singida, Songwe, Mbeya, Tabora, Iringa, Shinyanga, Njombe,Simiyu, Ruvuma, Mara, Mtwara, Mwanza, Lindi, Kagera, Pwani, Geita, Tanga,Kigoma, Kilimanjaro, Katavi, Atrusha, Rukwa, Manyara, Zanzibar na Dar es Salaam.



"Baada ya Dodoma Kongamano la Uponyaji kwa ajili ya Kuliombea Taifa na Serikali litaendelea Februari 21 hadi 23, 2020 katika ukumbi wa Akwa Vitae Hotel mkoani Singida hivyo Watanzania wote bila kujali imani, kabila au rangi njooni tukamuombea Mungu kwa ajili ya Taifa letu,"alisema Nabii Joshua.

No comments:

Post a Comment