Katika hali ya kawaida herufi huunda neno na maneno huunda sentensi nayo sentensi huunda kikundi cha maneno. Kwa kawaida neno ni tamko mojawapo miongoni mwa mengi ambalo mtu hulitamka katika mchakato wa mazungumzo unaopelekea iwepo misemo ambayo ni fungu la maneno yenye maana mahususi ili kutoa fundisho kwa jamii.
Kwa mantiki hiyo, semi ni maneno yanayozungumzwa na watu yanayoleta maana mahususi katika lugha inayozungumzwa katika eneo fulani. Kiswahili ikiwa lugha ya Taifa la Tanzania kimekuwa pia lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na lugha ya Umoja wa Afrika (AU). Bila kusahau kuwa ni lugha ya kufundisha katika shule, taasisi na vyuo vikuu katika mataifa mbalimbali duniani.
Watafiti wa mbalimbali duniani katika tafiti zao wanabainisha kuwa lugha ya Kiswahili inashika nafasi ya kumi katika lugha elfu sita zinazozungumzwa na watu wengi duniani ambapo kwa nchi za Afrika kinashika nafasi ya pili kwa kuongelewa na watu wengi Barani humu.
Tafiti wa wataalamu wa lugha kutoka Umoja wa Nchi za Afrika unabainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2063 lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa lugha kuu ya mawasiliano katika nchi zote za Afrika.
Ukuaji na utambuzi huu wa Kiswahili katika Afrika na duniani kote unaipa heshia Tanzania ikiwa ndio kitovu cha Kiswahili kuwa lugha maridhawa, adhimu na yenye ubora wa kipekee yenye msamiati unaofaa kufundishia mataifa mbalimbali duniani.
Tanzania ikiwa nchi Mama kwa lugha hiyo, haina budi kuwa mstari wa mbele katika kutumia maneno ya Kiswahili sahihi na fasaha. Kutokana na sababu hiyo, Serikali imeamua kusisitiza matumizi sahihi ya Kiswahili haswa katika misamiati yake.
“Kumekuwa na matumizi mabaya ya maneno ‘Kisimbuzi’ na ‘King’amuzi’ Serikali haiwezi kufumbia macho watu au taasisi ambazo zinaharibu matumizi sahihi ya maneno haya ama kwa makusudi ama kwa kutofahamu.”Anasema Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri Mwenye dhamana ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Dkt. Mwakyembe ameendelea kulipigia chapuo suala hili kwenye ziara zake za kikazi katika mikoa Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mwanza, Singida na Tanga ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wadau wa habari pamoja na wa utamaduni.
“Watanzania tuwe mfano kwa kutumia Kiswahili fasaha ili kuudhihirisha ulimwengu kuwa Kiswahili kitovu chake ni Tanzania.” Aliongeza Waziri Mwakyembe katika ziara zake alizozifanya hivi aribuni.
Aidha, akiwa katika kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na Chama cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili Vyuo Vikuu na vya Kati Tanzania (CHAWAKITA) Januari 4, 2020
katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) cha jijini Mwanza, Dkt. Mwakyembe alibainisha umuhimu wa vyombo vya habari vya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kusimamia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Kwa umahiri wa hali ya juu Waziri Mwakyembe alitoa somo la Kiswahili kwa matumizi sahihi ya maneno haya huku washiriki wakimsikiliza kwa umakini na shabaha ya Serikali ni kuwa baada ya ufafanuzi huo makosa yaliyokuwa yakifanyika awali kutojirudia.
Alisema kuwa kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili neno “Kisimbuzi” lina maana ya kifaa kinachotumika kufichua alama za kielektroniki zilizofichwa ili ziweze kusikika na kuonekana kupitia kwenye simu, televisheni, faksi na intaneti kwa kutumia mfumo wa dijiti.
Aliongeza kuwa kamusi hiyo hiyo neno “King'amuzi” maana yake ni kifaa kinachotumika kufichua vitu vilivyofichwa au kupotea aghalabu mabomu yaliyofukiwa ardhini, madini na vito vya thamani au ni kitu kinachotambua vitu au hali ya hatari kama vile moshi, moto na mazingira mengine ya hatari.
Waziri Mwakyembe alisisitiza kuwa imezuka kasumba ambayo imejengeka miongoni mwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili vikiwemo vyombo vya habari ambavyo vinatumia vibaya lugha ya Kiswahili ama kwa makusudi ama kwa kutokujua kutumia.
“Kupitia kongamano hili, naliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuvionya mara moja baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vinara wa matumizi mabaya ya neno ‘king’amuzi’ badala ya neno ‘kisimbuzi’.” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Ni ukweli usiopingika ukisikiliza vyombo vya habari vya redio, televisheni na magazeti pamoja na mitandao ya kijamii ikiwemo Face Book, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya kijamii. Maneno haya ‘Kisimbuzi’ na ‘King’amuzi’yanatumika ndivyo sivyo, ni vema vyombo vya habari vichukue nafasi yake ya msingi ya kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya maneno hayo.
Katika kongamano hilo, Waziri Mwakyembe alikuwa Mgeni Rasmi ambapo alisisitiza kuwa nafasi ya Lugha ya Kiswahili kuwa kati ya Lugha kumi bora duniani, kuna haja kubwa ya kuithamini, kutunza na kuiendeleza ili ikue zaidi.
Kutokana na uhitaji wa lugha ya Kiswahili kwa mataifa mengine, Watanzania wanafursa ya kusoma lugha hiyo ili kupata wataalamu wa kukifundisha Kiswahili sanifu na fasaha, uhariri na ukalimani. Hii ni fursa kwa wakufunzi, wahadhiri, wataalamu waliopo katika sekta ya Kiswahili ama wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosoma somo la Kiswahili kuchukua hatua za makusudi ili waweze kuingia kwenye kada mbalimbali zilizopo kwenye ya lugha ya Kiswahili.
Pia alitilia mkazo juu ya umuhimu wa wajuzi wa lugha yetu kujua kutumia vyombo vya kisasa vya kufundishia lugha ya Kiswahili katika muktadha mbalimbali iwe vyuoni, kwenye ukalimali na maeneo mengine.
Miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo ni Mwakilishi wa BAKITA ambaye pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) Dkt. Nestory Ligembe alimshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Waziri mwenye dhamana na Lugha ya Kiswahili Dkt. Harrison Mwakyembe kwa uongozi wao thabiti ambao umeleta mafanikio makubwa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Akisoma risala kwa niaba ya Chama cha Wanafunzi na Wahitimu wa Kiswahili Vyuo Vikuu na Vya Kati Tanzania (CHAWAKITA) tawi la SAUT Mwenyekiti wa chama hicho Tumaini Masanja amesema kuwa wanawajibu wa kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, kukuza vipaji vya wanafunzi katika lugha ya Kiswahili, kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati katika suala la kuithamini na kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuitangaza ndani na nje ya nchi.
Kongamano liliongozwa na kauli mbiu “Kiswahili Urithi wetu kwa maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania kwa kuwa chimbuko lake ni Tanzania” kwa lengo la kuendeleza kampeni ya kukuza na kuendeleza Kiswahili.
Ni muda muafaka sasa kila mwenye taaluma ya Kiswahili aone ana mchango katika kukuza, kuhifadhi na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Soko la lugha hii adhimu sasa limevuka mipaka ya nchi za SADC zikiongozwa na Afrika Kusini iliyoonesha uhitaji wa walimu wa Kiswahili.
Rais Dkt. Magufuli ameonesha njia, ni wakati sasa wa kutumia fursa hiyo, wakati ndio huu, tumia Kiswahili katika kukuza uchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja na hatimaye uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment