Friday, February 21, 2020

NAIBU KATIBU MKUU UWT TAIFA AMPONGEZA RITTA KABATI, AKERWA NA VIONGOZI “WACHUMIA TUMBO”



Naibu katibu mkuu wa UWT Taifa, Jesca Mbogo amempongeza mbunge viti maalum mkoa wa Iringa (CCM), Ritta Kabati kwa jitihada zake za kusaidia katika shughuli za maendeleo za mkoa wa Iringa.

Mbogo amesema hayo, wakati akikabidhi mifuko ya saruji aliyokabidhiwa mbunge Ritta Kabati kutoka shirika la Nyumba la Taifa walioitikia wito wa mbunge Kabati wa kukarabati shule na vituo vya Afya Iringa.

Pia, Bi. Mbogo amewataka viongozi wanaopokea mifuko hiyo ya saruji kufanyia kazi zilizopangwa za kukarabati shule za msingi na sekondari, vituo vya afya pamoja na zahanati zilizokuwa zimeahidiwa na mbunge Kabati.

Aidha Mbogo amewataka wadau kuwachukia viongozi aliowataja kwa jina la “Wachumia tumbo”, wanaofanya kazi kwa maslahi yao binafsi huku wakiacha wananchi katika mazingira magumu.

Mbogo ameeeleza kuwa ipo haja ya wananchi pamoja na wapiga kura kuacha mazoea ya kuchagua mtu kwa kufahamiana na badala yake waweze kupima uwezo wa mtu katika kutekeleza yale aliyoyaahidi.

Nae mbunge Ritta Kabati amewapongeza shirika la nyumba la Taifa, kwa kukubali kutoa mifuko hiyo 100 huku akiyataka mashirika na taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Kabati ametaja ukosefu wa miundombinu bora mashuleni na katika vituo vya afya kama changamoto zinazotakiwa kutazamwa kwa kina kutokana na watoto kusoma katika mazingira magumu wakati wa mvua na baridi.

Akiongea kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika la nyumba la Taifa, meneja wa shirika hilo Iringa, ndg. Rebson Josia amempongeza mbunge Ritta Kabati kwa kuthubutu kushirikisha wadau wa maendeleo katika shughuli za maendeleo za mkoa wa Iringa.


Ndg. Josia amesema shirika la nyumba la Taifa liko tayari kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwajengea maisha bora wanyonge.

No comments:

Post a Comment