Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kulia) akiwa na mwenyeji wake ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe George Kahema Madafa mara baada ya kuwasili katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Roma, Nchini Italia tarehe 13 Februari 2020 ikiwa ni siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa 43 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza na Mshirika wa wa Idara ya Usimamizi wa Programu ya Makamu wa Rais wa IFAD Shekh Mbalozi Donal Broun, Nchini Italia tarehe 13 Februari 2020 ikiwa ni siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa 43 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe George Kahema Madafa wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Roma, Nchini Italia tarehe 13 Februari 2020 ikiwa ni siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa 43 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akimkabidhi zawadi ya Kahawa Balozi wa Tanzania nchini Italia Mhe George Kahema Madafa mara baada ya kuwasili katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Roma, Nchini Italia tarehe 13 Februari 2020 ikiwa ni siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa 43 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD). Mwingine pichani ni Afisa Kilimo Mkuu Daraja la kwanza Bi Jaqueline Mbuya
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Roma-Italy
Mkutano wa 43 wa Magavana wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Jijini Roma nchini Italia umemalizika kwa magavana hao kukubaliana kwa kauli moja juu ya kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030.
Kutoka nchini Tanzania Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa IFAD ni miongoni mwa mashirika muhimu ambayo yanaonyesha ushirikiano jadidu na nchi za Afrika hususani Tanzania.
Amesema kuwa IFAD inafadhili mipango ya kimaendeleo na ambayo ni muhimu kwa masikini zaidi kati ya masikini duniani na ambao wanaishi vijijini pembezoni kabisa mwa miji.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika mkutano huo zimeeleza kluwa takribani asilimia 70% ya watu duniani mara nyingi wamesahuliwa na wenye kuhitaji msaada mkubwa hivyo miongoni mwa maamuzi yao ni kuhuisha uwezekano wa mashirikiano maradufu ili kuwasaidia wananchi masikini kote Duniani.
Amesema kuwa hivi karibuni, serikali kwa kushirikiana na IFAD zimeanzisha na kuunda mpango wa fursa za mkakati wa nchi (COSOP) 2016-2021 na walikubali kufanya kazi pamoja katika kubadilisha sekta ya kilimo nchini Tanzania katika sekta ndogo kama mimea, mifugo na uvuvi.
Waziri Hasunga amesema kuwa IFAD imekuwa mshirika muhimu katika mipango ya ujenzi na fedha na miradi ambayo inalenga kupambana na umasikini katika maeneo ya vijijini na kuimarisha uwezekano wa kumaliza njaa kwa jumla. Ambapo imekuwa mbele katika kubadilisha shughuli za kilimo katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Tanzania.
Waziri Hasunga ameeleza shukrani za Tanzania kwa IFAD kwa miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikitekelezwa katika nchi ya Tanzania huku akisisitiza kuwa serikali haitosubiri mpaka mwaka 2030 kumaliza njaa bali itafanya haraka iwezekanavyo kumaliza baa la njaa.
Amesema juhudi hizo ni kwa ajili ya kushughulikia changamoto za umasikini wa watu waishio vijijini kupitia mikakati ya maendeleo ya hali ya juu na mipango ya ukuaji wa uchumi.
Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuendeleza ushirikiano maradufu baina yake na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ili kuhakikisha kuwa inaendana na lengo la Jumuiya ya Kimataifa ya kufuta baa la njaa Duniani ifikapo mwaka 2030.
Kadhalika, Mhe Hasunga ametoa wito kwa nchi za Kiafrika wa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kupambana na wimbi kumbwa na wahamiaji sanjari na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani katika ujumla wake.
Taarifa iliyotolewa na mfuko huo imeutaka Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo barani Afrika na kwamba hiyo itasaidia kupunguza wimbi la uhamiaji kuelekea Ulaya.
IFAD ni Shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo ya kilimo, ambalo ni shirika la Umoja wa mataifa kwa ajili ya maendeleo vijijini lililoanzishwa tarehe 13 Desemba 1977 kwa lengo kufanya ukue uzalishaji wa kilimo na vyakula haki kufikia kwa ngazi ya maisha ya kujitosheleza.
MWISHO
No comments:
Post a Comment