Mbunge wa Viti maalum Kundi la Wananawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Mwanza Mhe Kiteto Koshuma amewakabidhi mradi wa mashine ya kutotolea vifaranga vya kuku na fedha taslimu kwaajili ya uendelezaji wa vikundi vya UWT kwa kata 19 za wilaya ya Ilemela maarufu kama Fogong’o ili wanawake hao waweze kujikwamua kiuchumi.
Akiwa katika kikao cha Baraza la Umoja wa Wanawake lililofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba Ilemela likiwa na lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 kutoka kwa madiwani wa Viti Maalum wa wilaya hiyo, Mhe Kiteto amesema kuwa anawapongeza wanawake hao kwa kushiriki uchaguzi wa mamlaka za Serikali za mitaa na kukipatia ushindi chama cha mapinduzi kwa zaidi ya asilimia 98% wilayani humo huku akiwataka kuendelea kuzitumia fursa za mikopo inayotolewa na manispaa na ile ya sekta binafsi kwaajili ya uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi
‘Ndugu zangu tumshukuru sana Mbunge wetu wa Jimbo la Ilemela kwa kutuletea wataalamu na wawezeshaji kutoka benki ya Azania, Tuitumie fursa hii vizuri na mie kama mbunge wenu wa Viti maalum nimewaletea mashine ya kutotolea vifaranga kama mradi wa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi ..’ Alisema
Aidha Mhe Kiteto amepongeza kazi kubwa inayofanywa na mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula juu ya utekelezaji wa Ilani sanjari na kuwataka wanawake hao kuendelea kumuunga mkono na kumtia moyo ili iwe rahisi kutimiza majukumu yake.
Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa wanawake wilaya ya Ilemela Bi Salome Kipondya amemshukuru mbunge huyo wa viti maalum kwa mchango wake katika kuwaunga mkono wanawake hao wenye lengo la kuwakwamua kiuchumi sambamba kumpongeza mbunge wa jimbo la Ilemela kwa kazi kubwa anayoifanya katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ikiwemo ujenzi wa mradi wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa kituo cha afya Buzuruga, kituo cha afya karume, ujenzi wa barabara ya sabasaba-kiseke-buswelu, barabara ya nyakato-buswelu, miradi ya mikubwa ya maji, elimu, urasimishaji makazi na maendeleo ya jamii.
Baraza la UWT wilaya ya Ilemela lilihudhuriwa na katibu wa UWT mkoa wa Mwanza Bi Mary Mhoha na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji na baraza wa mkoa wa Mwanza.
No comments:
Post a Comment