Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua miche ya michikichi wakati alipotembelea kitalu cha mbegu bora zinazooteshwa katika kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma, Februari 21, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Filson Kagimbo kuhusu uoteshaji wa mbegu bora za michikichi wakati alipotembelea kitalu cha miche ya michikichi cha kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichpo wilayani Kigoma, Februari 21, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Dkt. Filson Kagimbo (wa pili kushoto) kuhusu uoteshaji wa miche bora ya michikichii alipotembelea kitalu cha kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma, Februari 21, 2020. Kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba na wanne kushoto ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako. (PIcha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika uzalishaji wa mbegu bora za zao la michikichiki katika kituo cha Tari Kihinga mkoani Kigoma.
Aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Frbruari 21, 2020) alipotembelea kituo cha utafiti wa zao la michikichi cha Tari Kihinga kilichopo wilayani Kigoma alipokuwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Kigoma.
Akiwa kituoni hapo, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utafiti juu ya uendelezaji wa zao la michikichi uliliyofanywa na TARI kuanzia mwaka 2018, ambapo hadi kufikia Februari 15, 2020 taasisi hiyo ilikuwa imezalisha mbegu 1,525,017 ambazo zinaweza kupandwa katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30,500.
Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, hivyo ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ziada itakayobakia itauzwa nje ya nchi.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hasa vijana kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa upo uhakika wa kupata mbegu bora na pia zao hilo litawakwamua kiuchumi na kuwaondolea umasikini wa kipato.
Pia, amewaagiza Maofisa Ugani kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwaelekeza namna ya kulima zao hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji mashamba, matumizi bora ya pembejeo ili waweze kulima kisasa na kujiongezea tija.
Baada kutembelea kituo hicho Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwanga Community Centre uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka watumishi wa umma watenge muda ya kusikiliza kero za wananchi.
“Watumishi mnatakiwa kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi. …hamuendi na kama mngekuwa mnaenda kusingekuwepo na mabango kwani kitendo cha kuwepo mabango ni ishara tosha kwamba hamuendi.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani Kigoma za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo sh bilioni 4.6 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji inapata sh milioni 50 kila mwezi hivyo hakuna sababu ya wananchi kukosa dawa.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya karibu na makazi ya wananchi zikiwemo za afya ili kuwapunguzia kutembea umbali mrefu hadi hospitali za wilaya au mkoa.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Baraza lake la Madiwani wahakikishe wanasimamia vizuri matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo.
Waziri Mkuu alikemea tabia ya baadhi ya wananchi katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma kudai fidia kwenye maeneo hata ya mapori na kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya kanda, aliwataka wabadilike.
Awali, Waziri Mkuu alishiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Mujahidina uliopo eneo la Buzebazeba mijini Kigoma, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaasa waumini wa dini ya kiislam na wananchi kwa ujumla kuendelea kushikama na kulinda amani.
Pia, Waziri Mkuu aliwahamasisha walime zao la michikichi kwani Serikali imeamua kulifufua zao hilo ili waweze kuondokana na umasikini. Wanaotamani kulima michikichi wajiandae wakati utakapofika watasambaziwa miche.
No comments:
Post a Comment