WATANI wa jadi, Simba SC na Yanga wamegawana pointi baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo, Simba SC inafikisha pointi 35 katika mchezo wa 14, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 10 zaidi ya mahasimu wao hao wa jadi, ambao hata hivyo wamecheza mechi 12 tu.
Katika mchezo wa leo, mabingwa watetezi Simba SC ndiyo walioanza kupata kupata bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere.
Kagere alifunga bao hilo dakika ya 42 kwa penalti ya utata iliyotolewa na refa Jeonisia Rukyaa baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondan kumvuta kwa mkono Mnyarwanda huyo nje kidogo ye boksi, lakini akaenda kuangukia ndani.
Wachezaji wa Yanga SC walilalamikia adhabu hiyo wakimuambia refa madhambi yalifanyika nje ya boksi, lakini mwanamama huyo hakubadili uamuzi wake.
Dakika ya kwanza tu baada ya kuanza kipindi cha pili Simba SC wakafanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa kiungo Deogratius Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akimalizia pasi ya Kagere.
Kiungo mpya, Balama Mapinduzi akaifungia Yanga SC bao la kwanza kwa shuti la umbali wa mita 30 baada ya kumpokonya mpira kiungo wa wapinzani, Muzamil Yassin dakika ya 49.
Wakati Simba bado wanajiuliza, Yanga SC wakafanikiwa kusawazisha bao la pili kupitia kwa kiungo wake, Mohamed Issa ‘Banka’ dakika ya 53 akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto, Adeyoum Ahmed.
Baada ya hapo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kosa kosa za pande zote mbili, huku makipa wa timu zote, Aishi Salum Manula wa Simba na Mkenya Farouk Shikhalo wa Yanga wakifanya kazi nzuri.
Wafungaji wote wa mabao ya pili hawakumaliza mchezo huo baada ya kuumia akianza Deo Kanda wa Simba SC ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Dilunga dakika ya 52 na Mohammed Issa wa Yanga aliyempisha Deus Kaseke dakika ya 69.
Wachezaji watatu walionyeshwa kadi za njano, mabeki Juma Abdul na Ally Mtoni ‘Sonso’ wa Yanga na Kagere wa Simba SC.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Paschal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda/Hassan Dilunga dk52, Muzamil Yassin, Meddie Kagere/ John Bocco dk69, Clatous Chama na Francis Kahata.
Yanga SC; Farouk Shikhalo, Juma Abdul, Adeyum Ahmed/ Andrew Vincent ‘Dante’dk64, Kelvin Yondan, Ally Mtoni ‘Sonso’, Abdulaziz Makame/ Yikpe Gislein dk62, Mohammed Issa ‘Banka’/ Deus Kaseke dk69, Mapinduzi Balama, Ditram Nchimbi, Papy Kabamba Tshishimbi na Haruna Niyonzima.
No comments:
Post a Comment