Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma leo ambapo aliwataka kuwajibika ipasavyo mahali pa kazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwasili katika ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika leo jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Watumishi la Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika leo jijini Dodoma na kufunguliwa na Waziri Mussa Azzan Zungu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amemtaka kila mtumishi katika Ofisi hiyo kuwajibika ipasavyo mahali pa kazi na kuepuka kujihusisha na vitendo visivyokuwa vya kimaadili. Zungu ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo ambapo aliwakumbusha kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuimarisha utendaji kazi ili kufanikisha dhana ya
Tanzania ya viwanda.
“Ninafahamu kwamba watumishi wana malalamiko yanayohusu kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na upungufu wa watumishi katika Idara na Vitengo, malalamiko haya ni mtambuka katika Wizara zote kwani yametokana na uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari na ualimu zoezi lililoendeshwa na Serikali kuanzia mwaka 2016. Ninawasihi muwe na subira wakati Serikali ikiimarisha mifumo yake ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Zungu alibainisha kuwa Baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu mahali pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi hivyo aliwataka kuendeleza ushirikiano ili kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Ofisi na Taifa kwa ujumla.
“Watumishi wenzangu hakikisheni mshahara mnaopewa mnautendea haki! Msitake kupata mshahara wa bure! Fanyeni kazi kwa bidii” Zungu alisisitiza.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa Mabaraza ya Wafanyakazi katika Taasisi ni takwa la Kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Idara na Ofisi ambapo malengo yake ni kuhakikisha kuwa majukumu yanatekelezwa ipasavyo, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga mazingira bora ya kazi, maslahi ya watumishi na kusimamia haki na ustawi
katika sehemu za kazi.
Aliwakumbusha kuwa wajibu wa Mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na kuzingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi.
Agenda na madhumuni ya mkutano huu ni kutoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha nusu mwaka cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/20.
No comments:
Post a Comment