Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi baada ya kufunga semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26, 2019. Kulia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko , Wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Stanslaus Nyongo na wapili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
Baadhi ya washiriki wa semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofunga semina hiyo kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina ya Viongozi wa Dola katika Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali Madini baada ya kuifunga semina hiyo kwenye ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Januari 26, 2019. Waliokaa kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Profesa. Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na kulia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Stanslaus Nyongo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinawalinda wafanyabiashara wa madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata sheria na kujiepuka kamata kamata zisizo na tija.
“Katika kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu.”
Ametoa agizo hilo leo (Jamapili, Januari 26, 2020) wakati akifunga semina ya ushiriki wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatakiwa vitumie Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuviagiza vyombo vya Dola kusimamia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha kuwa masoko yote ya madini nchini yanalindwa.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba kila taasisi ina utaalamu na wataalamu wake. Kwa hivyo, hatunabudi kufanya kazi kwa kuheshimu na kutambua utaalamu ama taaluma za wengine tunaoshirikiana nao.”
“Sasa ni vema tukaondoa tofauti zetu na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuimarisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali madini. Aidha, tutambue kuwa kuna nyakati hatuhitaji kutumia nguvu nyingi bali ushauri tuu ili kutatua changamoto husika.”
Waziri Mkuu ameelekeza kwamba kuanzia sasa wadau wote wanaopatikana na madini wapewe utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza madini hayo badala ya kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni.
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa yote ya Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema walikosa msaada wa kitaalamu. “Ni wajibu wetu sote kama watumishi wa umma kujenga mazingira rafiki ya kazi, kuaminiana na kufanya kazi kwa ushirikiano.”
Wakati huo huo,Waziri Mkuu amesema kuazia sasa suala la migodi kutegemea bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi lifikie ukomo kwa kuhakikisha kuwa, kila huduma inayohitajika migodini, inapatikana nchini.
Waziri Mkuu amesema nchi inawajibu wa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa madini kwa maana ya kutoa huduma kwa ubora stahiki na kwa wakati muafaka.
Amesema sekta ya madini inazalisha ajira ila kuna changamoto ya ubora wa ajira, mishahara na stahiki katika kazi zinazofanana na suala la unyanyasaji wa wafanyakazi.
Waziri Mkuu amesema masuala mengi hapo yanaweza kuonekana haraka kwenye maeneo yao ya kazi, hivyo ni vyema wakawa na taarifa hizo kwa wakati na kuwasilisha kwa wahusika ili mambo yawekwe sawa na kuipeleka sekta mbele.
Akizungumzia kuhusu suala la unyanyasaji wa wafanyakazi wazalendo amesema si suala la kufumbiwa macho kama ilivyo suala la usalama wa watenda kazi katika migodi.
Kadhalika, suala la udhibiti wa wageni kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania wenzetu pia ni jukumu letu na hivyo ni wajibu wetu kusimamia mikataba tuliyoingia na wawekezaji hususani eneo la urithishaji wa madaraka na ujuzi kwa wazawa.
Kwa upande wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Waziri Mkuu amewaagiza watafute suluhu ya changamoto ya usalama wa wafanyakazi kipindi wakiwa kazini na baada ya kumaliza muda wa kazi kwa hiari au kwa kustaafu au kumaliza mkataba. “Tumepokea malalamiko mengi sana katika eneo hilo.”
“Hivyo, ni wajibu wetu kushirikisha wadau wote wanaohusika na masuala ya ajira, bima za wafanyakazi, afya za wafanyakazi na usimamizi wa stahiki za wafanyakazi kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto hii ili isiendelee kukomaa.”
Vilevile, Waziri Mkuu ameagiza suala la utunzaji wa mazingira liwekewe mkazo wa kipekee maana nje ya mazuri yote yaletwayo na Sekta ya Madini, uharibifu wa mazingira unaweza kugharimu maisha ya binadamu, wanyama na mimea.
Waziri Mkuu amesema “mazingira yetu ndio uhai wetu sisi na vizazi vijavyo, hivyo ni wajibu wetu kama Wizara kuhakikisha wawekezaji wetu ni watu wema kwa mazingira yetu.”
Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu mkubwa alioufanya ambao umeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya madini.
“Hili linadhihirishwa na kitendo cha utiaji saini makubaliano ya uanzishwaji wa Kampuni ya Twiga Minerals uliofanywa juzi Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Januari 2020 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017.”
Awali, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja kwenye masuala ya usimamizi wa sekta ya madini nchini.
Alisema suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini linafanyika kwa kushirikiana kati Wizara ya Madini na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwamba wanaendelea kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza.
Waziri Biteko ametumia fursa hiyo kutuma salamu kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa madini bandia pamoja na wanaotaka kuuza madini nje ya mfumo kuwa zama zao zimekwisha.
No comments:
Post a Comment