Monday, January 27, 2020

VYOMBO VYA ULINZI VYATAKIWA KUANDAA MTANDAO WA USIMAMIZI MADINI NCHINI

Baadhi ya washiriki wa Semina kutoka Vyombo vya Ulinzi na Ulasama Mkutano wa
Wizara wakifuatilia semina hiyo inayoendelea katika ukumbi wa St. Gaspar jijini
Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza kwenye
Semina kuhusu Ushiriki wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Usimamizi na
Udhibiti wa Rasilimali Madini
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza kwenye Semina jambo katika semina
inayohusu Ushiriki wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kusimamia na kudhibiti
rasilimali madini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu , Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Watu Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama akizungumza jambo wakati akifungua
Semina kuhusu Ushiriki wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama iliyovishirikisha vyombo
hivyo kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimetakiwa kuandaa Mtandao wa
Kusimamia Rasilimali Madini Nchini hususan kwenye udhibiti wa Utoroshaji
rasilimali hizo kutokana na mchango wa vyombo hivyo katika ukuaji na
Maendeleo ya Sekta ya Madini.

Aidha, vimetakiwa kuweka mazingira salama ya wawekezaji katika sekta
husika ili kuhakikisha waliopo wanaendelea kufanya shughuli zao vizuri bila
kubugudhiwa huku vikitakiwa kuhakikisha mazingira salama yatakayovutia
wawekezaji wapya katika Sekta ya Madini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu
, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama
mapema leo Januari 25, 2020 Jijini Dodoma, wakati akifungua Semina
kuhusu Ushiriki wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Usimamizi na
Udhibiti wa Rasilimali Madini.

Mhagama amesema kuwa, mabadiliko makubwa ya Kisera, Sheria, na
Taratibu yaliyofanyika katika Sekta ya Madini yamepelekea mabadiliko
makubwa katika mageuzi ya Sekta ya Madini huku akimpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kuwezesha na
kusimamia mabadiliko hayo na kuipongeza Wizara ya Madini kwa
usimamizi dhabiti ambao umewezesha mafanikio yanayoonekana katika
sekta ikiwemo uanzishwaji wa masoko ya madini.

Vilevile, amewataka washiriki hao kuhakikisha wanatoka na maazimio
kutoka katika semina hiyo, ambayo yataendelea kuivusha Sekta ya Madini
katika kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 huku akiitaka
Wizara ya Madini kuandaa semina kama hiyo kwa Vyombo vingine vya
Ulinzi na Usalama na Taasisi nyingine za Umma ikiwemo Uhamiaji, taasisi
zinazohusika na masuala ya ajira, Halmashauri za Wilaya na Majiji na
wadau wengine muhimu katika sekta ya madini lengo likiwa ni
kuifungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine.

‘’ Kazi yetu ni moja tu, kuhakikisha tunafungamanisha sekta hii na sekta
nyingine ili kuhakikisha sheria na taratibu zote zilizowekwa katika sekta hii
zinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu,’’ amesema Waziri Mhagama.
Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika semina hiyo
amesema kwamba, Wizara iliona ipo haja ya hukakikisha wasimamizi wote
wa Sekta ya Madini wanakutana ili kuwa na uelewa unaofanana katika
usimamizi wa sekta ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza manufaa
zaidi kwa sekta husika.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana mara baada ya kufanyika kwa
marekebisho ya Sheria ya Madini ameeleza kuwa, ni pamoja na
kuimarishwa kwa usimamizi kwenye Sekta ya Madini hali iliyopelekea
kuvuka kwa lengo la makusanyo kwa kipindi cha Nusu mwaka wa Mwaka
wa Fedha 2019/20 ambapo Wizara imekusanya kiasi cha shilingi bilioni
242 sawa na asilimia 103, na kuongeza kuwa, yamechagizwa na
ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wa madini vikiwemo vyombo vya
ulinzi na usalama.

Pia, Waziri Biteko amesema kuwa, mapato na uzalishaji wa madini
mbalimbali ikiwemo dhahabu, almasi na tanzanite yameongeza nchini
tofauti na ilivyokuwa awali na kusema kuwa, thamani ya madini ya
dhahabu kwenye soko la Geita imefikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni
238 kwa nusu mwaka tofauti na awali huku madini ya tanzanite
yakiiwezesha serikali kukusanya mapato ya shilingi bilioni 2 baada ya
kujengwa ukuta kuzunguka migodi ya tanzanite Mirerani kutoka
makusanyo ya shilingi milioni 71 kabla ya kujengwa kwa ukuta.

Ameongeza kuwa, uzalishaji wa madini ya almasi katika Mgodi wa Mwadui
Shinyanga umeongezeka kufikia karati Laki Nne ukiwa ni uzalishaji
mkubwa tangu kuanzishwa kwa mgodi huo, na hivyo kuyafanya madini
hayo kuwa ya pili katika uchangiaji wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali
yakiongozwa na madini ya dhahabu ambayo yanachangia kwa asilimia 86.
‘’Ndugu washiriki yapo mafanikio mengi yanayoonekana katika sekta hii, na
yote yamechangiwa na championi wa mabadiliko hayo ambaye ni Rais Dkt.
John Magufuli,’’ amesema Waziri Biteko.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amevipongeza vyombo hivyo
kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Sekta ya Madini na
kueleza kuwa, Wizara imejipanga kuhakikisha vyombo hivyo katika ngazi
zote vinafikiwa ili kupatiwa elimu kuhusu sekta husika.

Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Utawala na Rasilimali Watu,
Benedict Mwakulyamba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini, amemweleza Waziri Mhagama kuwa, vyombo hivyo ambavyo
vinasimama kama daraja katika usimamizi wa rasilimali hivyo vitahakikisha
vinasimamia rasilimali hiyo ili kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya
taifa.

Huku akinukuu kauli ya Rais Dkt. John Magufuli kwamba ‘Tanzania si
maskini’ amesema itaungwa mkono na vyombo hivyo kwani inatoa dira na
mwelekeo wa usimamizi wa rasilimali madini katika kuhakikisha kwamba
Tanzania inakuwa nchi inayojitegemea kutokana na uwepo wa rasilimali
madini.

Awali, akizungumza katika semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini
Prof. Simon Msanjila amesema kuwa, semina hiyo imelenga katika kujadili
na kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo ili kuboresha na
kuongeza tija zaidi.

Semina hiyo ya Siku mbili inayofanyika Jijini Dodoma inavishirikisha
vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama kutoka Mikoa yote nchini.

No comments:

Post a Comment