Thursday, January 2, 2020

Viongozi wa Dini Rukwa Kupewa Mbinu za Kukabiliana na Ukatili Dhidi ya Watoto


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na mkewe Veronica Wangabo wakiwasalimia watoto waliohudhuria ibada ya kuukaribisha mwaka 2020 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristu Mfalme Sumbawanga mjni.

*******************************

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema ili kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, serikali haina budi kufanya kazi kwa karibu na viongozi wote wa dini wa madhehebu mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kuwataka kuwa karibu na watoto ili watoto hao wawe huru kuwataarifu viongozi hao aina yoyote ya manyanyaso wanayoyapata wakiwa nyumbani.

Amesema kuwa kwa muda mrefu katika mkoa watoto wamekuwa wakiathirika kutokana na ugomvi baina ya wazazi na hatimae kutopata mapenzi ya baba na mama hali inayopelekea watoto hao kutopata malezi mazuri ya kifamilia na hatimae kuishia mitaani na kuwa na kizazi kisichofaa katika jamii na kusisitiza kuwa serikali ya mkoa imejizatiti kupambana na hali hiyo.

“ Chimbuko la maisha yetu wote liko kwenye familia na familia ni watoto, kwahiyo tujielekeze zaidi katika malezi ya watoto wetu, lakini pia kuhakikisha ya kwamba tunawapa na kuheshimu haki zao, haki za watoto tunakwenda kuzifungua kwa watoto wetu wote kama serikali, tutawaelimisha watoto haki zao, tutawaambi wakifanyiwa manyanyaso waende kwa nani, waripoti kwa nani matatizo hayo,” Alisema

“lakini narudi kwa viongozi wa dini na wenyewe tutawaomba wawe karibu sana na watoto ili watoto waweze kufunguka wawaambie manyanyaso wanayoyapata majumbani, nasi tutashirikiana na viongozi wa dini kupambana na hayo manyanyaso na huo ukatili wa watoto” Alisisita.

Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa akitoa salamu zake za mwaka mpya katika ibada ya kuukaribisha mwaka 2020 iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristu Mfalme, mjini Sumbawanga.

Mwishoni mwa mwaka 2019 ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa ulizindua mpango mkakati wa wa miaka mitano wa kukabiliana na kupambana na mimba za watoto pamoja na kupunguza watoto wa mitaani, mpango ambao utekelezaji wake unaanza mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment