Thursday, January 30, 2020

MABWAWA YA UMWAGILIAJI YALIYOPUNGUA KINA KUTAFUTIWA MUAROBAINI-MHE MGUMBA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 31 Januari 2020 wakati wa mkutano wa kumi na nane Jijini Dodoma. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) amewahakikishia watanzania kuwa serikali imekusudia kuhakikisha kuwa mabwawa yaliyopungua kina yanakuwa na maji na kuwa na uwezo wa kufanya kazi.

Mhe Mgumba ameyasema hayo tarehe 31 Januari 2020 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Chilonwa Mhe Joel Mwaka Makanyaga ambaye alitaka kufahamu serikali ina mpango gani kukabiliana na mabwawa ya umwagiliaji yaliyopungua kina katika kijiji cha Buigiri, Chalinze na Izava.

Amesema kuwa Bwawa la Buigiri ambalo lipo katika Kata ya Buigiri lilijengwa mwaka 1960 likiwa na uwezo wa kumwagilia hekta 40 na kunyweshea mifugo. Bwawa hilo limekuwa likijaa mchanga na tope kutokana na mafuriko na hivyo kupungua kwa kina cha maji.

Pamoja na Serikali kukarabati bwawa hilo katika kipindi cha mwaka 2005 na mwaka 2009 kwa kuongeza kina kwa mita moja bado bwawa hilo liliendelea kujaa mchanga na tope kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika juu ya bwawa na kusababisha mchanga natope kujaa bwawani.

Mhe Mgumba amesema kuwa Tathmini iliyofanyika mwaka 2012 ilionesha kuwa bwawa hilo linahitaji ukarabati wa sehemu ya kutoroshea maji (spillway) na kunyanyua tuta ili kuongeza kina kwa gharama ya Shilingi milioni 475.

Amesema kuwa Bwawa la Ikowa lililopo katika kijiji cha Chalinze na Ikowa lilijengwa mwaka 1959 kwa ajili ya kupata maji ya mifugo na kumwagilia jumla ya hekta 96 kati ya hekta 220 katika skimu ya Chalinze.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, bwawa hilo limekuwa likijaa mchanga na tope kila msimu wa mvua na hivyo kusababisha  athari katika Tuta na kupungua kwa kina cha maji katika bwawa hilo.

Bwawa la Izava lilijengwa miaka ya 1972/73 kwa ajili ya mifugo na kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na changamoto ya kujaa mchanga na matope bwawa hilo liliendelea kutoa huduma kwa wananchi hadi mwaka 2015 ambapo kupitia mradi wa TASAF lilikarabatiwa na  wananchi  kupitia utaratibu wa kufanya kazi za kujitolea na kutumia kiasi cha Shilingi 7,418,000/= kuwalipa wananchi hao. Mwaka 2017/18 wakati wa mvua za msimu kingo za bwawa hilo zilibomoka na hivyo kushindwa kutunza maji kwa ajili ya kilimo.

Kadhalika, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba, akijibu swali la Mbunge wa Solwa Mhe Ahmed Ally Salum kuhusu Bwawa la Ishololo katika Kata ya Usule na Misengwa ni mabwawa ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa muda mrefu sasa nlakini wizara imeomba maombi maalum ili kupata fedha za kukamilisha miradi hiyo miwili.

Amesisitiza kuwa wizara ya kilimo imejipanga kuhakikisha kuwa inasimamia miradi ya umwagiliaji iliyoshindwa kukamilika kwa wakati kabla ya kuanza miradi mingine mipya.

MWISHO

No comments:

Post a Comment