Saturday, January 11, 2020

MABULA AKABIDHI HATI MIA MOJA ZA KIMILA KWA WAKULIMA WADOGO KIJIJI CHA LITOA RUVUMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiangalia nondo zinazotumika kwenye ujenzi wa mradi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  katika eneo la Mpepo wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma jana wakati akikagua mradi huo. Kulia ni  mhandisi wa Mradi kutoka NHC Omar Chitawala.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akifafanua jambo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba na Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye shamba la miti la Mpepo lililopo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya na aliyekunja mikono ni Mhandisi wa Mradi kutoka Omar Chitawala.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Kimila Bibi Dafrosa Komba wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa katika wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Songea Pololeti Mgema.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi waliokabidhiwa Hati za Kimila wakati wa zoezi la kutoa hati katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Songea Pololeti Mgema.

********************************
Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekabidhi hati mia moja za Kimila kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa kilichopo katika jimbo la Peramiho wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma na kuwataka wamiliki wake kuzitunza na kuzitumia hati hizo kujiletea maendeleo.


Akizungumza wakati wa kuwakabidhi hati hizo katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini akiwa kwenye shughuli za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi ya ujenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa katika mikoa ya kusini jana, Naibu Waziri Mabula aliwataka wakulima waliokabidhiwa hati kutouza ardhi zao kwa nia ya kupata fedha za haraka.


‘’Mmepiwa msikimbilie kuuza ardhi bila kufuata taratibu kwa tamaa ya kupata fedha za haraka maana mkiuza mnaweza kupunjwa fedha’’ alisema Dkt Mabula.


Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji ili kuwa na salama za miliki za ardhi zilizoainisha maeneo ya shule, soko, maeneo ya kuabudia, viwanja vya michezo pamoja na maeneo ya uwekezaji.


Dkt Mabula alizitaka pia halmashauri kuandaa maeneo ya uwekezaji sambamba na kuhaulisha maeneo ili kuwa rahisi kwa Mwekezaji atakayekuja kuwekeza katika sekta mbalimbali na kusisitiza kuwa ili kuwaendeleza wananchi kiuchumi ni lazima ardhi ipimwe na kufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Vijijini Pololeti Mgema aliupongeza Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa juhudi kubwa iliyofanya kufanikisha wakulima wadogo kupata hati miliki za kimila na kubainisha kuwa wilaya yake imejifunza bila kushirikisha wadau zoezi la kuwapatia hati wakulima wadogo lingechukua muda mrefu.


 Naye Mratibu wa MVIWATA katika mkoa wa Ruvuma Laila Haji alisema Asasi yake iliona umuhimu wa wakulima wadogo kuwa na salama za miliki za mashamba yao na ndiyo maana ikafanya juhudi kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Songea ili kuwapatia hati wakulima wa kijiji cha Litoa.


Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo kwa wakulima na wananchi kwa ujumla katika suala la hati miliki za ardhi ni elimu ndogo kuhusiana na masuala hati za ardhi, mfumo dume kwa wanawake kumiliki ardhi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) uliopo Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma. Mradi huo pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa nyumba na ofisi za TFS katika maeneo mbalimbali nchini unajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

No comments:

Post a Comment