Thursday, January 9, 2020

MABULA AISHUKIA HALMASHAURI YA MTAMA KWA KUWA NA VIWANJA 105 KWA MIAKA 40


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili Halmashauri ya wilaya ya Mtama wakati wa ziara yake ya kuamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi mkoani Lindi jana, wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama Samwel Gunzar na Kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Lindi Majid Myao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Methew Makwinya  akizungumza wakati Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokutana na viongozi pamoja na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Mtama wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi katika mkoa wa Lindi jana.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mtama wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi mkoani Lindi jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimueleza jambo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Baptista Kihanze (Kulia) wakati wa ziara yake ya kuamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika mkoa wa Lindi jana, kushoto kwa Naibu Waziri ni Afisa Ardhi wa Manispaa Endrew Munisi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa jana wakati wa ziara yake ya kuamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika mkoa wa Lindi. Kulia ni Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa wa Lindi Majid Myao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi Andrea Chezue akizungumza katika kikao baina ya viongozi wa halmashauri yake na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati Naibu Waziri alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi katika mkoa wa Lindi jana,
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi ikiwa ni muendelezo wa ukaguzi wa miradi inayofanywa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini. Kushoto ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini Mpoki Mwalufunda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa mpango kazi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi na Msimamizi wa mradi huo Fadhili Pazi jana.
(PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

........................
Na Munir Shemweta, WANMM LINDI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameishukia idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mtama mkoa wa Lindi kwa kuwa na viwanja 105 tu vilivyopimwa na kumilikishwa kwa wananchi ikiwa ni takriban miaka 40 tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo mwaka 1980.



Akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Lindi jana, Dkt Mabula alisema pamoja na halmashauri hiyo kuwa ya siku nyingi lakini imeshindwa kupima maeneo na kuwamilikisha wananchi jambo lililosababisha hadi leo kuwa na hati 105 pekee.



Alisema, kutomilikisha wananchi viwanja mbali na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi lakini  kunasababisha wananchi kutokuwa na miliki za viwanja vyao na hivyo kuwakosesha fursa ya kujiendeleza kiuchumi kupitia hati za ardhi ambazo zingeweza kutumika katika kuchukulia mikopo benki.


‘’Halmashauri ina viwanja 105 wakati ni ya siku nyingi inaonesha watumishi wa sekta ya ardhi hawafanyi kazi yao ipasavyo, hapa kuna uzembe, Mkurugenzi fuatilia suala hili vifaa vya upimaji vipo katika Kanda tatizo ni nini? ‘’ alisema Dkt Mabula


Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alishangazwa na halmashauri  ya Mtama ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja imeandaa hati mbili tu za ardhi jambo alilolieleza kuwa linampa mashaka na utendaji wa watumishi wa sekta hiyo katika halmashauri hiyo.


Ameiagiza ofisi ya Ardhi Kanda ya kusini kuiangalia halmashauri ya wilaya ya Mtama na kuisaidia katika masuala ya ardhi ikiwemo kupima maeneo ili kuwa na idadi kubwa ya viwanja vilivyopimwa.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mtama Methew Makwinya na Mbunge wa jimbo la Mchinga mkoani Lindi Hamidu Bobali walimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa, eneo kubwa katika halmashauri hiyo halijapimwa na kubainisha kuwa njia pekee ya kuwasaidia wananchi wa Mtama ni kuwapatia timu ya wataalamu watakaosadia kupanga, kupima na kumilikisha maeneo na hatimaye kutoa hati zikiwemo za kimila.


Walimuomba Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kungalia namna fukwe zilizopo kwenye halmashauri hiyo zitawanufaisha wamilki wake kwa kuwapatia hati zitakazoweza kuwaisadia kiuchumi.


Akiwa mkoani Lindi Naibu Waziri Mabula aitembelea pia halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na Manispaa ya Lindi ambapo katika halmashauri ya Ruangwa alikagua masijala ya ardhi na kubaini majalada ya hati takriban mia tatu yakiwa hajakamilishwa kwa ajili ya kutoa hati kwa wamiliki wake kwa muda mrefu. Kufuatia hali hiyo Dkt Mabula ameipa miezi mitatu idara ya ardhi katika halmashauri ya Ruangwa kuhakikisha inawatafuta na kuwamilikishi waombaji wote na kupatiwa taarifa kuhusiana na suala hilo.


Kwa upande wa Manispaa ya Lindi Dkt Mabula alisikitishwa na Manispaa hiyo kushindwa kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi pamoja na wadaiwa hao kupelekewa lani za madai. Kwa mujibu wa Afisa Ardhi wa Manispaa ya Lindi Andrew Munisi ofisi yake ilipeleka jumla ya hati za madai 245 zenye thamani ya bilioni 3 ambapo baadhi ya wadaiwa wamelipa na kiasi kisocholipwa ni bilioni moja.


Naibu Waziri Mabula pia katika ziara yake hiyo alikagua miradi ya ujenzi ya Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) katika wilaya za Ruangwa na Nachingwea na kuridhishwa na ujenzi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) aliouelezea kuwa pamoja na kwenda kwa kasi lakini unazingatia viwango na ubora. 

No comments:

Post a Comment