Wednesday, January 8, 2020

“Kwa mchango huu wa milioni 500 wa NFRA, umeonyesha kuwa si Taasisi ya kupoteza fedha za Serikali” – Waziri Mpango

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Milton Lupa akiwa kushoto kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wengine wakishuhudia tukio la makabidhiano ya hundi ya mfano ambayo NFRA imetoa kama mchango wake ni Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Msajiri wa Hazina Bwana Athumani Mbuttuka na wa mwisho kulia ni Mhasibu wa NFRA Bi. Anna Msemwa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Milton Lupa akipongezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wengine wakishuhudia tukio la makabidhiano ya hundi ya mfano ambayo NFRA imetoa kama mchango wake ni Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Msajiri wa Hazina Bwana Athumani Mbuttuka na wa mwisho kulia na Mhasibu wa NFRA Bi. Anna Msemwa.
 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akimpongeza Mhasibu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi. Anna Msemwa wengine wakishuhudia tukio la makabidhiano ya hundi ya mfano ambayo NFRA imetoa kama mchango wake ni Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Msajiri wa Hazina Bwana Athumani Mbuttuka na Mtendaji Mkuu wa NFRA, Bwana Milton Lupa.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Msajiri wa Hazina Bwana Athumani Mbuttuka, Naibu Katibu Mkuu (Uchumi), Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Adolf Ndunguru pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Utawala) Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga na nyuma waliosimama ni Mtendaji Mkuu wa NFRA, Bwana Milton Lupa pamoja na Mhasibu Bi. Anna Msemwa (Leo) katika jengo la HAZINA, Jijini Dodoma.



Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema mchango wa fshilingi milioni 500 zilizotolewa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo kwenye hafla ya makabidhiano ya michango na magawio kutoka kwa Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali kimeonyesha kuwa Taasisi hiyo inajiendesha kwa faida na tija; na kwamba inapaswa kupongezwa.

Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati wa hotuba yake, baada ya kupokea gawio na michango ya fedha zilizotolewa kwa Serikali kutoka kwa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi 13 za Serikali kwenye hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kilimanjaro katika Jengo la Wizara ya Fedha, Jijini Dodoma leo.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo imetoa mchango wake wa shilingi milioni 500 kwa Serikali mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ambaye aliambatana na Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Msajiri wa Hazina Bwana Athumani Mbuttuka.

Akiongea wakati wa hafla hiyo ya makibidhiano ya hundi za mfano, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema inatia moyo kuona Wenyeviti wa Bodi pamoja na Wakuu wa Taasisi, Wakala na Mifuko na Vyuo vya Elimu ya Juu ambao wameo gawiwo na michango yao kwa Serikali, yenye jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 2.

“Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru kwa kuitikia wito wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, nataka niwahakikishe kuwa fedha hizi, zitarudi kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia Watanzania wanyonge”. Amekarirwa Waziri Mpango.

“Wito wangu na matarajio yangu ni kuwa mwaka ujao, mtajiangalia zaidi ili tupate zaidi kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi wetu”.

Waziri Mpango ameongeza kuwa kwa sasa duniani nchi zilizokuwa zikitoa misaada kupitia Mfuko Mkuu wa Dunia (Global Fund) hazifanyi hivyo, zaidi zimejikita katika kutoa misaada hiyo kwa nchi zao zaidi na kwamba ndiyo maana ni lazima nchi zinazoendelea kama Tanzania zijifunge mkanda kwa kutumia rasilimali zao.

“Misaada siku hizi imepungua, ni aibu kwa Baba mwenye nyumba, kwenda kwa Wakubwa na kuanza kuombaomba, ndiyo maana Rais wetu ameamua kutumia rasilimali za ndani, kuendeleza Taifa letu lenye utajili wa rasilimali, ikiwemo rasilimali Watu”.

“Namaliza kuwa kusema, Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa zile Taasisi Thelasini na Sita (36) zilizobaki ambazo hazijatoa gawio na michango yao, tarehe 23 Januari, 2020 saa 6 usiku, wasingoje barua kutoka kwangu, tarehe 24 Januari, 2020 wasiwepo Ofisini, Tanzania yenye Watu zaidi ya milioni 55; hatutakosa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi kuchukua nafasi zao, katika jambo hili, hakuna utani” Amemalizia Waziri Mpango.

Akiongea baada ya hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Milton Lupa amesema, amefurahishwa kuona NFRA imetii agizo la Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa mchango wa shilingi milioni 500 ambapo fedha hizo, zinaenda kwenye miradi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Napenda kuwapongeza Watumishi wote wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa pamoja, tumefanikisha jambo hili, furaha yangu ni kuwa michango hii, inaenda kwenye miradi ya kimkakati, ambapo Taifa zima tutanufaika kwa rasilimali zetu”. Amekaririwa Bwana Lupa.

No comments:

Post a Comment