Tuesday, December 3, 2019

WAZIRI HASUNGA ASISITIZA ULAZIMA WA KUWA NA VIWANDA VYA MBOLEA NCHINI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa mbolea chenye lengo la Kuweka Mikakati ya Kutumia Fursa za Uwekezaji katika Viwanda vya Mbolea Nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es salaam, tarehe 3 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha wadau wa mbolea chenye lengo la Kuweka Mikakati ya Kutumia Fursa za Uwekezaji katika Viwanda vya Mbolea Nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es salaam, tarehe 3 Disemba 2019.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa mbolea chenye lengo la Kuweka Mikakati ya Kutumia Fursa za Uwekezaji katika Viwanda vya Mbolea Nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es salaam, tarehe 3 Disemba 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Serikali imesema kuwa inathamini sana mchango wa Sekta binafsi katika kukuza uchumi kwani ndio chanzo kikubwa cha Pato la Taifa kutokana na mchango wake kupitia kodi, ushuru na tozo mbalimbali.

Kilimo ni moja ya Sekta zinazoongoza kwa ushiriki wa sekta binafsi. Wakulima wote ni sekta binafsi. Ukiondoa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), wafanyabiashara wote wa mazao ya Kilimo ni sekta binafsi.

Aidha, wauzaji wote wa mbolea isipokuwa kampuni ya mbolea Tanzania (TFC) ni sekta binafsi. Vile vile, viwanda vyote 13 vinavyotengeneza mbolea (Fertilizer) na visaidizi vya mbolea (Fertilizer supplements)  vinamilikiwa na sekta binafsi.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 3 Disemba 2019 wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa mbolea chenye lengo la  Kuweka Mikakati ya Kutumia Fursa za Uwekezaji katika Viwanda vya Mbolea Nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es salaam.

Mhe Hasunga amesema kuwa ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo ni dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa inaanzisha viwanda mbalimbali nchini huku akisema kuwa kwa Wizara ya Kilimo msukumo maalumu ni kuhakikisha kuwa viwanda vya kuzalisha mbolea vinaanzishwa hapa nchini.

Amesema kuwa Tanzania ina viwanda 10 vya mbolea ambavyo hutengeneza virutubisho vya aina mbalimbali kwa ajili ya mimea kama vile (Nitrogen - N, Phosphorus - P, Potassium - K, NP, NK, PK, NPK n.k.)

Amesema baadhi ya wafanyabashiara walioko nchini wana mitambo ya kuchanganyia mbolea (Fertilizer Blending) ili kupata aina za virutubisho mahsusi kwa ajili ya mazao (Crop Specific Fertilizer Catalogues) na pia kuwekewa visaidizi vya mbolea kwa ajili ya kurekebisha afya ya udongo (Soil Specific Fertilizer Catalogues).

Amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa viwanda vitatu vya visaidizi vya mbolea (Calcium/gypsum n.k.) ambavyo hutumika kurekebisha hali ya  udongo ili mbolea ichukuliwe vizuri na mmea (optimal fertilizer uptake). Hata hivyo, uzalishaji wa viwanda hivi bado ni mdogo na hivyo kutokidhi mahitaji makubwa ya mbolea Nchini kwetu.

Ili kuimarisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kuwa na bei rafiki kwa wakulima ni lazima kuongeza uwezo wa viwanda vya mbolea, viwanda vya visaidizi vya mbolea na mitambo ya kuchanganyia mbolea ili viwe na uwezo wa kutosheleza mahitaji ya wakulima nchini.

Pia amesema inatakiwa kujenga viwanda vipya vya mbolea, viwanda vya visaidizi vya mbolea na mitambo ya kuchanganyia mbolea ili viwe na uwezo wa kutosheleza mahitaji ya wakulima.

Zingine ni kuweka mkakati wa miaka mitano wa kupunguza au kuondoa kabisa uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi; kuweka mkakati wa miaka miaka mitano wa kupunguza bei ya mbolea kwa mkulima kutokana na utengenezaji wa mbolea ndani ya nchi; na Kuweka mkakati wa kuongeza uuzaji wa mbolea nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji ya Nchi hizo na kuiongezea Serikali pato la fedha za kigeni.

Pia, Taasisi zinazotoa huduma kwenye tasnia ya mbolea (fedha, utafiti, elimu, usafirishaji, nishati, vyama vya ushirika) kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba zinaweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika viwanda vya mbolea.

Mhe Hasunga amesema kuwa pamoja na hayo lakini pia Asasi za kiraia (AZAKI) zinatakiwa kuwa mstari wa mbele kufuatilia na kuona kwamba wadau wote wanashiriki katika mchakato wa kuhakikisha viwanda vya mbolea vinakuwepo nchini.

Kadhalika amesema kuwa hizi sio zama za kusubiri matamko ya Serikali na kuanza kuyakosoa bila kupendekeza majawabu. AZAKI zinatakiwa kuwa sehemu ya kutafuta majawabu badala ya kutafuta changamoto bila kutafuta au kupendekeza majawabu.

MWISHO

No comments:

Post a Comment