Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt.
Angelina Lutambi akizungumza na timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya
Jamii wakati timu hiyo ilipofika mkoani hapo kwa lengo la kukisanya
maoni kutoka kwa wadau wa Maendeleo ya Waanwake na Jinsia katika
kuboresha Sera yao.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera
na Mipango sehemu ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sophina Mjangu akitoa maneno ya
awali kabla ya ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa maendeleo ya Wanawake
na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni katika
kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka
kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi.
Hanifa Selengu akifafanua jambo katika kikao kazi cha wadau wa maendeleo
ya Wanawake na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni
katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa
wa Singida ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw.
Stanslaus Choaji akifungua kikao kazi cha wadau wa maendeleo ya Wanawake
na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni katika
kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
*************************************
Na Mwandishi Wetu Singida
Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeamua kufanya tathimini ya
Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 200 na Mkakati wa
utekelezaji wa mwaka 2005 ili tathimini hiyo isaidie kufanya mapitio ya
Sera itakayozingatia makubaliano ya mikataba mbalimbali, Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa
miaka mitano na maoni ya wadau.
Haya yameelezwa
leo mkoani Singida na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango
sehemu ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sophina Mjangu wakati wa ufunguzi wa kikao
kazi kilichowakutanisha wadau wa maendeleo ya wanawake na Jinsia kutoka
mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora na Wizara.
Bi. Sophina
amesema kuwa madhumuni ya Sera iliyopo yalikuwa ni kutoa mwelekeo ambao
ungehakikisha kuwa mipango, Mikakati na shughuli mbalimbali za uongozi
na maendeleo katika kila Sekta na Taasisi inazingatia usawa wa kijinsia.
Ameongeza kuwa
lengo kuu la kupitia Sera hiyo ni kuifanya iendane na wakati na iwezi
kubeba mabadiliko yaliyojitokeza katika miaka kumi na tisa tangu
kandaliwa kwake mwaka 2000 ikiwemo changamoto katika utekelezaji wa Sera
hii ikiwemo mapungufu yake na nini kifanyike ili kuiboresha Sera ili
kueandana na wakati husika.
“Hii itatokana na
maoni ya wadau tutakayoyapata inawezekana ikawa mpya au tukabadilisha
na jina la Sera ili tunawasikiliza wadau ili nadhani yote yanawezekana”
alisema Bi. Sophina
Akifungua kikao
kazi hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala
Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw. Stanslaus Choaji amesema kuwa Kikao
hicho kinatarajia kufikia malengo ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa
masuala ya Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake katika kufikia
maendeleo jumuishi hususan katika Sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na
Masuala ya kifedha, uwezeshaji wa wanawake katika nafasi za uongozi na
siasa, mazingira na Uzazi na Afya ya Mtoto na kukusanya Taarifa na
Takwimu zitakazowezesha kuandaa Rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake
na Jinsia.
Ameongeza
kuwa kikao kazi hicho kitawezesha kukusanya maoni yatayowezesha kuwa na
Sera Shirikishi inayozingatia masuala yote muhimu na kupata uelewa wa
pamoja kuhusu wajibu wa Serikali na wadau katika uwepo wa Sera ya
maendeleo ya Wanawake na Jinsia .
Naye Afisa
Maendeleo ya Jamii mkoa wa Singida Bw. Jonathan Simiti amesema kuwa Sera
hiyo inatakiwa kufanyiwa maboresho ingawa kuna juhudi za Serikali
katika kuondokana na Unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa hivyo Sera
isaidie wanawake kuwezeshwa katika kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Nimesikia
kwenye redio kuwa wanawake sasa wanaendesha magari makubwa kama malori
na mabasi ya abiria masuala ya kijinsia yamekuwa kwa kiasi kikubwa
nchini ukilinganisha na wakati uliopita” alisema Bw. Simiti.
Kwa upande
wake Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Singida Bi. Shukranui Mbago amesema
kuwa Sera iliyopo ni nzuri na inatekelezeka ingawa kuna mambo muhimu
yanatakiwa kuingizwa ikiwemo umiliki wa mali na kutoa maamuzi kwa watoto
wa kike na wanawake katika ngazi ya Kata.
“Unakuta
Mwanamke au mtoto wa kike anatafuta pesa lakini kwa asilimia kubwa
zinamilikiwa na wanaume na watoto wa kiume tunahitaji Sera isisitize
umiliki wa mali na utoaji wa maamuzi hasa katika Kaya kwa mtoto wa kike
na mwanamke” alisema Bi. Shukrani.
Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika machakato
wa kukusanya maoni kwa wadau kutoka Kanda saba za Tanzania Bara ili
kuwezesha maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka
2000.
No comments:
Post a Comment