Wednesday, November 27, 2019

VIONGOZI WA USHIRIKA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUONGEZA USHIRIKIANO

Dodoma, 
VIONGOZI katika Sekta ya Ushirika kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zazibar wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika sekta hii ili kuweza kubadilishana uzoefu wa namna bora ya jinsi ya kusimamia na kuimarisha vyama vya ushirika hapa nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa kikao kati ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bara (TCDC), Dkt. Benson Ndiege na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba, kilichofanyika Jijini Dodoma leo Jumanne, Novemba 27, 2019.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba ambaye ameambatana na Viongozi wa Taasisi ya fedha ya Ushirika Zanzibar Faraja Union Limited (Financial Access Reliability by Joint Action – FARAJA) yupo katika ziara Tanzania Bara kutembelea na kujionea mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya vyama vya ushirika vinavyofanya vizuri katika mikoa ya Dar Es Salaam, Dodoma na Iringa.
Akiongea katika kikao hicho, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bara (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amewapongeza viongozi kutoka Zanzibar kwa uamuzi wao wa kufanya ziara ya kujifunza na kupata uzoefu kutoka Tanzania Bara kwenye vyama vya ushirika vinavyofanya vizuri ili waweze pamaoja na mambo mengine kuiendesha kwa mafanikio Taasisi ya FARAJA.
“Vyama vya Ushirika ni taasisi nzuri na zina manufaa makubwa kwa Wanaushirika, tatizo ni baadhi ya viongozi wanaoviendesha na kuvisimamia vyama vya ushirika kutokuwa waaminifu na waadilifu, hivyo lazima viongozi wa Ushirika tuweke mfumo mzuri wa kusimamia vyama hivi,” amesema Dkt. Ndiege.
Dkt. Ndiege amewataka viongozi wa ushirika kutoka Zanzibar kujifunza na kujielimisha kutokana na mafanikio na changamoto watakazojionea kwenye uendeshaji wa vyama vya ushirika watakavyovitembelea hapa nchini ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (TFC) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT).
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba, amesema kuwa lengo la ziara yao kama viongozi wa Serikali wanaosimamia Sekta ya Ushirika Zanzibar na viongozi wa Taasisi ya FARAJA limeleta matumaini makubwa kutimia kwa kuwa wameweza kubadilshana mawazo na uzoefu na viongozi wenzao wa Tanzania Bara kwenye uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika.
“Tumejifunza mengi na tumepata darasa zuri, kwa kubadilishana mawazo na kubaini baadhi ya sababu zinazotufanya tusiweze kupata mafanikio makubwa katika uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika katika maeneo yetu,” amesema Khamis David Simba, Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar.
FARAJA ni taasisi ya fedha inayoundwa na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Vyama vya Uzalishaji na Vikundi vya Wajasiliamali vilivyosajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika ya Zanzibar. Taasisi hii inaendeshwa kwa kufuata misingi na kanuni za ushirika na Inafanya kazi Zanzibar (Unguja na Pemba).

No comments:

Post a Comment