Wednesday, November 27, 2019

TANTRADE YASAIDIA KAMPUNI 31,891 KUPATA TAARIFA ZA BEI YA MASOKO NA BIDHAA

Naibu Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Bi. Latiffa Mohammed, akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani), kuhusu Mafanikio ya TANTRADE kwa maiaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Habari-MAELEZO, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Bi. Latiffa Mohammed, akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani), kuhusu Mafanikio ya TANTRADE kwa maiaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Habari-MAELEZO, Jijini Dar es Salaam.

Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.
……………..
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuziunganisha kampuni 31,891 kuweza kupata taarifa za bei na  masoko ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano (Novemba 27, 2019) Jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya Taasisi hiyo katika Kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Novemba 2015 hadi Novemba 2019.
Alisema kuwa ya wafanyabiashara hao, TANTRADE iliweza kuunganisha katika masoko wafanyabiashara  405 na kuuza tani 102,000 za mahindi, tani 2,000 za karanga, tani 5,000 za soya, tani 50 za ufuta, tani 7 za majani ya papai, kilogramu 200 za unga wa ubuyu, tani 2 za iliki, tani 5,000 za muhogo na tani 3.2 za tangawizi ya unga.
Aliongeza kuwa miongoni mwa bidhaa zilizoonesha uhitaji mkubwa katika masoko ya nje ni pamoja na matunda, samaki na mazao ya bahari, jamii ya mikunde, asali, kahawa, chai, korosho, viungo na vyakula, ambapo maulizo ya bidhaa hizo yalitoka katika nchi za India, Nchi za Kiarabu, Misri, Marekani, Vietnam na Ulaya.
‘’Mbali na kusambaza taarifa za uhitaji wa bidhaa mbalimbali TANTRADE kwa kushirikiana na wanunuzi kutoka nchi zao tumewezesha kupatikana kwa muendelezo wa kimkakati wa kupenya katika masoko yao, semina mbalimbali ziliratibiwa ambapo wafanyabiashara na wadau 425 walishiriki ili kutambua fursa za masoko ya nje na taratibu za kuyafikia’’  alisema Latifa.
Kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa masoko ya nje ya nchi, Latifa alisema TANTRADE imeendelea kuratibu maonesho ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) kwa lengo la kutoa fursa za kutangaza bidhaa zilizoongezewa thamani na upatikanaji wa teknolojia ili kupanua wigo wa masoko ya nje ya nchi.
Latifa alisema kupitia DITF kila mwaka Tanzania hupokea wastani wa kampuni 500  kutoka zaidi ya nchi 35 zinazoshiriki maonesho hayo na hivyo kuwasaidia wafanyabiashara katika upatikanaji wa teknolojia na kusaidia kutatua changamoto za uzalishaji hafifu wa bidhaa za kilimo, uchenjuaji wa madini na hivyo kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.
Akifafanua zaidi Latifa alisema kwa mwaka 2019 pekee kupitia DITF, mafanikio mbalimbali yaliweza kupatikana ikiwemo kampuni 437 kupata oda ya kufanya biashara zenye thamani ya Tsh Bilioni 7.93, kufanyika kwa mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya wastani wa Tsh. Milioni 209, pamoja na kutengeneza ajira za muda mfupi zipatazo 14,912 zilizotokana na kazi mbalimbali za maonesho ikiwemo ujenzi, ulinzi na usafi.
Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya nje ya nchi, Latifa alisema Tanzania imefanikiwa kushiriki katika maonesho katika nchi zilizo na utengamano ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo wastani wa kampuni 200 zimeweza kushiriki na kutambua bidhaa zao kwenye nchi hizo na kuingia mikataba ya kibiashara ili kupata masoko endelevu.
Akitoa mfano Latifa alisema katika mwaka 2018/19, Tanzania ilishiriki maonesho ya 15 ya Biashara China ambapo kampuni 20 zilishiriki na kuweza kutafutiwa masoko ya bidhaa na kutangaza vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya utalii, mazao ya kilimo hususani kahawa, chai, karafuu, asali, korosho, mazao ya jamii ya kunde na bidhaa za mikono ikiwemo vikoi.
‘’Katika maonesho ya chakula ya Gulfood-Dubai kampuni tatu zaTanzania zilifanikiwa kutembelea maonesho hayo yaliyofanyika Dubai kwa lengo la kutambua fursa mbalimbali kutoka kwa washiriki, ambapo wanunuzi wa bidhaa mbalimbali kama asali kontena 30, kahawa tani 50, ukwaju tani 10 walipatikana’’ alisema Latifa.
Aidha Latifa alisema TANTRADE katika kutekeleza adhima ya Tanzania ya Viwanda ilianzisha maonesho ya bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayofanyika kila mwezi Desemba, ambapo tangu kuanza kwake mwaka 2007 wastani wa makampuni 497 hushiriki na kuwafanya wazalishaji wa bidhaa nchini kupata fursa ya kutambulisha bidhaa zao na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Tanzania.

No comments:

Post a Comment