Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea
kusimamia marufuku ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa
kushirikiana na Kikosi kazi cha Kitaifa. Kwa siku za hivi karibuni
kumekuwepo na wimbi la uzalishaji, utengezaji na uingizaji na usambazaji
wa mifuko isiyokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango
Tanzania (TBS).
Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuzuia
matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na Kamati za Mikoa na Wilaya
wanaendesha oparesheni maalumu nchi nzima kwa lengo la kusaka mifuko
isiyokidhi viwango.
Tarehe 30/10/2019 NEMC ilikamata
marobota 21 katika Wilaya ya Misenyi, Mkoani Kagera na marobota 7 Mkoani
Arusha ambayo yanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Arusha.
Upelelezi wa mashauri haya bado unaendelea.
Leo tarehe 4/11/2019 Baraza la
Taifa la Hifadhi na Usimamizi kwa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza wamekamata shehena ya
mifuko isiyokidhi viwango gunia 8 yenye thamani ya Shilingi
10,000,000/- Mifuko hiyo iliingia kupitia bandari bubu ya Bwiru jijini
Mwanza ikitokea nchi jirani. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani na
mifuko hiyo itateketezwa kwa mujibu wa sheria kama itakavyoelekezwa na
NEMC.
Ofisi ya Makamu wa Rais, inatoa
wito kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na
uuzaji wa mifuko mbadala kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Sheria.
Aidha, wafanyabiashara wanasisitizwa kuacha kuzalisha, kuingiza nchini,
kuuza na kusambaza mifuko isiyokidhi viwango. Hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya wote wanaokiuka agizo hilo.
No comments:
Post a Comment