Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akijadiliana jambo na Mbunge wa Jimbo la
Magu, Boniventura Kiswaga wakari wa ziara ya kukaga ujenzi wa mradi wa
maji wa Mji wa Magu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akimsikiliza Msimamizi wa ujenzi wa mradi
wa maji mji wa Magu, Mhandisi Wilbert Bujiku akielezea hatua
zilizofikiwa za ujenzi wake.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akitoa maelekezo wakati wa ziara yake
ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji Magu. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo
la Magu, Boniventura Kiswaga na kulia ni Msimamizi wa ujenzi wa mradi,
Mhandisi Wilbert Bujiku.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akitoa maelekezo wakati wa ziara yake ya
ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji Magu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na ujumbe aliyoambatana nao
wakimsikiliza msimamizi wa mradi, Mhandisi Wilbert Bujiku (hayupo
pichani) akiuelezea mradi.
Eneo la chanzo cha maji cha mradi wa Mji wa Magu ambapo kuna mitambo ya kuvutia maji yanayotoka ziwani.
**********************************
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa muda wa siku 14 kwa
Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC)
kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Mji wa Magu.
Ametoa agizo
hilo Novemba 22, 2019 alipofanya ziara kwenye mradi huo Wilayani Magu,
Mkoani Mwanza ili kujionea hatua ya ujenzi iliyofikiwa sambamba na
kuzungumza na Mkandarasi.
Mara baada ya
kutembelea eneo la chanzo cha maji na kituo cha tiba ya maji cha mradi,
Mhandisi Sanga alibainisha kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi na
kwamba tayari wananchi wameanza kupata huduma ya maji lakini yapo maeneo
machache ambayo bado hayajakamilika inavyopasa na hivyo kumtaka
Mkandarasi kuhakikisha anayakamilisha kwa muda aliyopangiwa.
“Mradi
unaridhisha umejengwa vizuri ila tu shida ninayoiona hapa kuna maeneo
machache bado hayajakamilishwa vizuri ambayo kitaalam tunaita ‘snags’
kama kuna pipe imechomoka, koki, kurudishia rangi, na vingine vidogo
vidogo. Maelekezo yangu ni kwamba ndani ya wiki mbili kuanzia leo
maeneo haya yakamilike,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Aliongeza
kuwa Mkandarasi amekwishafanya kazi kubwa na kwamba hizo chache
zilizobaki ahakikishe anazikamilisha haraka na kwamba baada ya siku hizo
14 awe amekabidhi mradi kwa Mamlaka ya Maji Mji wa Magu na awe
ameondoka kwenye eneo la mradi ili kuondokana na gharama mbalimbali za
usimamizi wake.
“Hata kama
hatumlipi mkandarasi kwa hizi kazi zilizobakia lakini gharama bado
zitakuwepo tu ikiwa ni pamoja na kulipa watendaji wetu ambao ni
wasimamizi wa mradi fedha za kujikimu na gharama zingine zikiwemo za
usafiri wa kuja kukagua kazi mara kwa mara na hivyo kutumia mafuta,”
alisema Mhandisi Sanga.
Aliongeza
kuwa fedha za ujenzi wa mradi ni za wananchi kwani zilitolewa na wadau
wa maendeleo ambao aliwataja kuwa ni Benki ya Maendeleo ya Ulaya na
Shirika la Maendeleo la Ufaransa kama mkopo wa masharti nafuu ambao
Serikali inapaswa kulipa.
Alitahadharisha
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli
haipo tayari kushuhudia matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na
kwamba haitowavumilia wakandarasi wanaochelewesha miradi kote nchini
bila sababu za msingi.
“Namshukuru
sana Mhe. Rais ambaye kimsingi ndio mtoaji wa fedha, tunasema fedha
imetolewa na wafadhili lakini ni mkopo wa masharti nafuu na hivyo
zitalipwa kwa kodi za wananchi, kwa hiyo tutahakikisha hata shilingi ya
mwisho inatumika vizuri na hatuwezi kumtazama Mkandarasi afanye
anavyojisikia yeye wakati wa kukamilisha mradi,” alisema Mhandisi Sanga.
Akizungumzia
maeneo ambayo hayajafikiwa na mradi na uhitaji upo, Mhandisi Sanga
alielekeza Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Maji Magu (MAUWASA) pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA)
wayafanyie kazi na kwamba kwa maeneo yatakayokuwa nje ya uwezo wao
wayawasilishe wizarani ili wananchi wote waliokusudiwa waweze kunufaika
na mradi huo.
Aidha,
alishukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Magu kwa kushirikiana
na Mbunge wa Jimbo la Magu, kwa ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa mradi
na kwa uhamasishaji walioufanya kwa wananchi waliokuwa wakidai fidia.
Kwa upande
wake Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga aliipongeza Serikali
ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maji ambao aliuelezea
kuwa ni mwarobaini wa kero ya muda mrefu ya upatikanajni wa huduma ya
maji safi na salama kwa wananchi wake.
Naye
msimamizi wa mradi kutoka MWAUWASA, Mhandisi Wilbert Bujiku aliahidi
kusimamia vyema utekelezaji wa maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu na kwa
wakati kama ilivyoelekezwa.
Aidha,
akiwasilisha taarifa ya mradi kwa ujumla, Mhandisi Bujiku alisema mradi
utanufaisha zaidi ya wananchi 120,000 na kwamba hadi hivi sasa jumla ya
kaya 4,911 tayari zimeunganishwa na wanapata huduma ya maji na kwamba
vituo 21 vya kuchotea maji pia vimejengwa maeneo mbalimbali kulingana na
idadi ya wakazi wa maeneo husika.
Aliongeza
kuwa mradi umehusisha ujenzi wa tenki la lita milioni mbili za maji,
ulazaji wa bomba kuu kutoka ziwani hadi kwenye tenki umbali wa kilomita
10.9 na bomba za usambazaji kwa wananchi umbali wa kilomita 67 na kwamba
umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 16.
No comments:
Post a Comment