Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb)
akijibu swali bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 6 Novemba 2019 wakati
wa mkutano wa kumi na saba
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo inafanya jitihada za kuongeza wawekezaji katika zao la nazi kwa lengo
la kumpatia mkulima soko la uhakika na bei nzuri.
Jitihada hizo ni pamoja na kutoa elimu katika mnyororo wa thamani wa zao la nazi ikiwa ni pamoja na
kuwapatia wakulima mashine za kukamua mafuta ya nazi.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameyasema hayo leo tarehe 6 Novemba 2019
bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Jimbo la Mafia Mhe Mbaraka
Kitwana Dau ambapo ameongeza kuwa hadi
kufikia tarehe 30 Septemba 2019 Vikundi vya Wajasiriamali vya Tujitegemee na
Kaza Moyo vimepatiwa mashine zenye uwezo wa kukamua mafuta ya nazi lita 400 kwa
siku ambapo lita moja huuzwa kati ya Shilingi 8,000 hadi Shilingi 10,000.
Aidha, Serikali inaendelea kutafuta masoko ya
mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi
kupitia vikundi na vyama vya ushirika.
Vilevile, Serikali inaendelea kuweka miundombinu ya usafiri kwa kuunda
kivuko kitakachowezesha kuunganishwa kwa usafiri kutoka Mafia hadi Nyamisati
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na hivyo kuwezesha wakulima wa Mafia kusafiri
na mizigo yao ya nazi kwenda Dar es Salaam ambako watauza kwa bei nzuri
katika masoko makubwa.
Mhe
Mgumba alibainisha kuwa sababu za kushuka kwa bei ya zao la nazi ni pamoja na; uwepo wa wanunuzi wachache wa nazi na
hivyo kutokuwepo kwa bei ya ushindani ikilinganishwa na misimu iliyopita; kupanda
kwa gharama za usafirishaji wa nazi kutoka Shilingi 2,800 miaka mitatu
iliyopita na kufikia Shilingi 5,500 kwa gunia lenye nazi 200 mwaka 2019;
kupungua kwa wanunuzi wakubwa wa viwanda vya mafuta na bidhaa za nazi.
Zingine ni kuongezeka kwa matumizi
ya bidhaa mbadala za nazi kama vile mafuta ya kula ya mawese toka nje, na matumizi
ya mafuta ya kupaka yasiyotokana na nazi; kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi
ya dola na kushuka kwa mfumuko wa bei toka asilimia 11 kwa mwaka 2006 mpaka
asilimia 4 mwaka 2018/2019; na kushuka kwa uzalishaji wa nazi nchini kutokana
na magonjwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo hayawavutii wawekezaji wa
ndani na wa nje kwa sekta ya viwanda vya kuchakata nazi kutokana na hofu ya
kukosa malighafi.
Mgumba
ameongeza kuwa Wastani wa Uzalishaji wa nazi nchini
Tanzania katika msimu wa 2018/2019 ulikuwa tani 530,000. Kutokana na uzalishaji
huo, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa uzalishaji wa nazi
tukifuatiwa na Ghana iliyozalisha wastani wa tani 366,183.
Serikali kwa kushirikiana na
Sekta binafsi imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo kidogo
cha utafiti wa nazi cha Chambezi kilichopo Wilayani Bagamoyo. Shamba hilo
litatumika kuzalisha miche bora ya minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa
kunyong’onyea kwa minazi (Coconut Lethal
Disease) na kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.
Aidha, Serikali inahamasisha
kilimo cha minazi katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini
ambapo msimu wa 2018/2019 ilizalisha jumla ya mbegu 11,000 na kusambazwa kwa
wakulima katika mikoa ya Rukwa na Mwanza.
Ili kuhakikisha kuwa
upatikanaji wa mbegu bora za zao la nazi nchini, Serikali inafanya mazungumzo
na Jumuiya ya Asia - Pasific Coconut
Community (APCC) ambayo hutunza “germplasm” ya minazi ili kuwezesha
upatikanaji wa mbegu bora za minazi yenye kuongeza tija ili kukuza pato la
wakulima.
MWISHO
No comments:
Post a Comment