Rais Dkt. John Magufuli akimuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) Charles Kichere wakati wa hafla ya kuwapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali wa Serikali aliowateua mwishoni wa wiki. Hafla hiyo
iilifanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaaam.
Rais Dkt. John Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu naUtawala Bora (THBUB) Mohamed Khamis
Hamad mara baada ya kumuapisha katika hafla ya kuwaapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali iliyofanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019).
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali katika
hafla iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mara
baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali katika hafla
iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.
Ibrahim Juma mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali
katika hafla iliyofanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019) Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akiteta jambo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
mara baada ya kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali aliwaoteua
mwishoni mwa wiki. Hafla hiyo ilifanyika leo Jumatatu Novemba (4, 2019)
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akisalimiana na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali (CAG) Charles Kichere muda mfupi kabla ya kuapishwa na
Rais Dkt. John Magufuli wakati wa hafla ya kuwaapisha Viongozi na
Watendaji mbalimbali. Hafla hiyo ilifanyika leo Jumatatu (Novemba 4, 2019)
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Magufuli akiwaapisha Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania wakati wa hafla ya kuwapisha iliyofanyika leo Jumatatu Novemba
4, 2019.
(PICHA NA MAELEZO)
*****************************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
4.11.2019
RAIS Dkt. John Magufuli amemtaka
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu mpya wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles
Kichere kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na
kutambua nafasi, wajibu na majukumu yake ili kuepuka mgongano na
mihimili ya Dola.
Akizungumza katika hafla ya
kuwaapisha Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali aliowateua
mwishoni mwa wiki, Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu (Novemba 4,
2019), Rais Magufuli alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) anapaswa kutambua wajibu wake na kutekeleza maagizo na
ushauri anapopewa na Viongozi wengine wa Mihimili ya Dola na sio
kubishana nayo.
Rais Magufuli alisema Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ipo kwa mujibu wa
Sheria na Katiba ya Nchi, hivyo mwenye mamlaka ya uteuzi (Rais) ana
uwezo kumuondoa madarakani mteule wake kulingana na madaraka aliyonayo
kupitia Katiba iliyopo hivyo jukumu alilonalo CAG ni kufanya kazi zake
pasipo na kuonea watu.
‘’Unapopewa kazi usibishane na
Mhimili mwingine, tambua wewe ni mtumishi wa umma kasimamie ofisi yako,
una nafasi kama CAG kwa mujibu wa sheria na Katiba, lakini ni vyema
ukatambua kuwa mwenye Serikali yupo pia kuna mihimili mingine ya Dola
usibishane nayo’’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alimtaka CAG
mpya Charles Kichere kuiangalia upya Ofisi hiyo kwa kuwa yapo mambo
mengi mabaya yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi aliyepita hivyo ni
vyema akashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili kufanyia
kazi udhaifu mbalimbali uliokuwa ukijitokeza ambao ulikuwa ukileta
taswira isiyo nzuri Ofisi hiyo.
Akitolea mfano Rais Magufuli
alisema baadhi ya watendaji wa Ofisi ya CAG wamekuwa wakilipwa pesa na
Ofisi hiyo kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi wa fedha katika Balozi za
Tanzania nje ya Nchi, lakini maofisa hao wanapofika katika Balozi hizo
wamekuwa wakiomba kulipwa fedha kwa mara ya pili.
Akizungumzia Majaji wapya 12 wa
Mahakama Kuu aliowateua, Rais Magufuli aliwataka Majaji hao kwenda
kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili Mahakama ikiwemo utoaji
wa haki kwa wakati ili kuweza kuwasaidia wananchi maskini, kwa kuwa
mamlaka waliyonayo ni makubwa katika kusimamia nafasi ya utoaji haki
duniani.
Aliongeza kuwa iwapo Mahakama
itafanya kazi zake kwa usahihi itaweza kusaidia vizuri Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kufanya kazi zake kwa urahisi na hivyo
kuwafanya wananchi kuweza kujenga imani na mhimili huo wa Dola.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa
Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alisema nyongeza ya majaji wapya 12 wa
Mahakama Kuu walioteuliwa na Rais watasaidia kuongeza kasi ya ufanisi wa
utendaji kazi wa Mahakama ambapo kwa sasa idadi ya Majaji hao itafikia
78, ukiondoa majaji 2 waliopo katika kazi maalum.
Prof. Juma aliwataka majaji hao
kufanya kazi kwa weledi na maarifa na kuzingatia miongozo na viapo vya
maadili na uadilifu wa kazi zao, kwani wananchi wana imani kubwa na
mahakama katika suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi hususani
wananchi maskini.
‘’Mnaanza kazi na mtambue kuwa
mnaaminiwa na vyombo vya dola na wananchi, upo utaratibu wetu
tuliojiwekea na kuusimamia, tumejipangia kusikiliza mashauri 220 kwa
mwaka pamoja na kutoa hukumu kwa wakati, yote haya mnapaswa kwenda
kuyasimamia’’ alisema Prof. Juma.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alisema Watanzania wana imani kubwa na
mhimili wa mahakama katika kusikiliza na kumaliza changamoto mbalimbali
ikiwemo kufanya uamuzi wa kesi mbalimbali ambazo baadhi yake
zinapochelewa kukamilishwa kwa wakati zimekuwa zikisababisha idadi kubwa
ya wafungwa katika magereza mbalimbali nchini.
‘’Hivi karibuni, Mhe Rais
alitembelea Gereza la Butimba na alijionea idadi kubwa ya wafungwa, wapo
wengine wapo kwa makosa yasiyo ya kwao na wale wasiohusika basi
mahakama iharakishe kesi zao ili nao waweze kuungana upya na familia
zao’’ Alisema Spika Ndugai.
Katika Hafla hiyo, Rais Magufuli
aliwaapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Majaji
12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) pamoja na Makamishina wa
Tume hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Kamishina wa Kazi pamoja na
Balozi wa Tanzania Nchini Kuwait.
No comments:
Post a Comment